Tafiti
Tume ya Taifa ya Uchaguzi hufanya tafiti kwa lengo la kupata taarifa maalumu ambazo hutumika katika kutekeleza majukumu yake.Mwaka 2010, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya utafiti katika Jumuiya ya nchi zilizopo Kusini mwa Bara la Afrika, ili kujua vigezo vingine vinavyoweza kutumika katika nchi hizo kwa lengo la kuchunguza mipaka na kugawa majimbo kwa ufanisi zaidi.
Baada ya utafiti huo, na kwa kuzingatia mashauriano na wadau mbalimbali, Tume ilitumia taarifa ya utafiti huo kuongeza vigezo vingine katika Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2010 na vigezo hivyo ni:-
(i) Hali ya kiuchumi;
(ii) Ukubwa wa Eneo la Jimbo husika;
(iii) Mipaka ya Kiutawala;
(iv) Jimbo moja lisiwe ndani ya Wilaya/Halmashauri mbili;
(v) Kata moja isiwe ndani ya majimbo mawili;
(vi) Mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu;
(vii) Mazingira ya Muungano;
(viii) Uwezo wa Ukumbi wa Bunge; na
(ix) Idadi ya Viti Maalum vya Wanawake.
Aidha, kwa kuzingatia Ibara ya 75(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, katika Uchaguzi wa mwaka 2015, Tume ilitumia vigezo vitatu tu ambavyo ni:
(i) Idadi ya Watu, ambapo Tume iliamua kuyagawa Majimbo yote yaliyokuwa na idadi ya watu zaidi ya 400,000;
(ii) Ukubwa wa ukumbi wa Bunge; na
(iii) Mipaka ya kiutawala.