Watumishi wa Tume wachangia damu, wafanya usafi Kituo cha Afya Makole kuadhimisha Wiki ya Utumishi
Imewekwa: June 22, 2023
Watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo tarehe 22 Juni, 2023, wamechangia chupa 14 za damu na kufanya usafi wa mazingira katika kituo cha Afya Makole kilichopo jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma nchini ambayo hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe 16-23 juni.
Watumishi hao wakiongozwa na Mkurugenzi
wa Idara ya Utawala na Raslimali Watu Bw. Leonard Tumua kwanza walifanya usafi
wa mazingira kwa kufyeka majani na kukusanya takataka katika maeneo mbalimbali
ya kituo hicho, na kufuatiwa na zoezi la kutoa damu.
Akizungumza mara baada ya
kukamilika kwa zoezi la kutoa damu, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makole
Dkt.Revocatus Bartazar amewashukuru watumishi hao kwa kuchangia kiasi hicho cha
damu kwani mahitaji ya damu katika kituo hicho kwa akina mama wanaojifungua ni
makubwa.
Amesema kwa mwezi akina mama 600
hadi 700 hujifungua katika kituo hicho na mahitaji ya damu ni makubwa kwani asilimia 10 ya akina mama wanaojifungua
hukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi
baada ya kujifungua.
Amesema sababu kubwa inayopelekea akina mama
wanaojifungua kupoteza maisha ni kupoteza damu nyingi baada ya kujifungua.
“Sababu kubwa inayopelekea vifo vya akina mama wanaojifungua nchini
Tanzania ni kutoka damu nyingi baada ya kujifungua,” amesema Dkt Bartazar.
Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia
90 ya vifo vitokanavyo na uzazi vinatokana na damu kutoka nyingi baada ya
kujifungua hivyo njia ya kupunguza vifo vya aina hiyo ni kwa wananchi
kujitokeza kuchangia damu kama walivyofanya watumishi wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi.
Amesema mama aliyepoteza damu
nyingi kutokana na kujifungua akipata chupa moja inamsaidia kuweza kurudisha
uhai wake, hivyo kwa watumishi hao kuchangia chupa 14 wameweza kuokoa uhai wa
akina mama 14 watakaohitaji damu .
Naye Mratibu wa Kitengo cha Damu
Salama wa Kituo hicho cha Afya Bw.Jerome Felician Marando amewapongeza
watumishi wa NEC kwa kuchangia chupa 14 za damu kwani amesema kiasi hicho ni
kikubwa kwani mara nyingi wanapofanya mazoezi ya kuhamasisha watu kuchangia
damu wanapata chupa 5 au 6 hivyo kupata chupa 14 ni kitu kikubwa sana kwa
mahitaji ya Kituo cha Afya Makole.
Kwa upande wake Mwakilishi wa
Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu Bi. Felister Ishuza amesema shughuli ya
usafi na kuchangia damu iliyofanywa na watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
ilikuwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo hufanyika kila
mwaka tarehe 16-23 juni.