Watendaji wa Uchaguzi Jimbo la Amani Zanzibar watakiwa kuzingatia katiba, sheria za uchaguzi
Imewekwa: November 16, 2022Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji wa uchaguzi katika Jimbo la Amini Tanzania Zanzibar kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano, sheria za uchaguzi na kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na maelekezo ya Tume.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume Mhe. Balozi Omari Ramadhani
Mapuri wakati akifungua mafunzo kwa
wasiamamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika Jimbo la
Amani yaliyofanyika tarehe 16 Novemba 2022, kwenye Ofisi za Tume zilizopo
Unguja.
Alisema sanjari na kuzingatia miongozo hiyo, Mhe. Balozi Mapuri
aliwaasa watendaji hao wa uchaguzi kuvishirikisha vyama vya siasa na wadau wengine
wa uchaguzi katika jimbo hilo ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao ya
uchaguzi.
Aliongeza kuwa uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na
taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa kwani hatua na taratibu hizo
ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri, wenye ufanisi na unaopunguza malalamiko na
vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
“Ni muhimu kwenu pia kuhakikisha mnayatambua na kuyajua vyema
maeneo ambayo chaguzi zitandeshwa ikiwemo miundombinu ya kufika katika kata na
vituo vya kupigia kura” alisema Balozi Mapuri nakuongeza kuwa:
“Pamoja na mambo niliyoyaanisha hapo awali, napenda
kuwasisitiza kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini
mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengola kuhakikisha mpangilio mzuri ambao
utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani”
Aliwataka watendaji hao kuhakikisha wanawaajiri watendaji wa
vituo wenye weledi, wanaojitambua na kwa kadri inavyowezekana waachane na
undugu au upendeleo kwa ndugu na jamaa wasio na sifa za kufanya shughuli za
uchaguzi.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge
katika Jimbo la Amani Tanzania Zanzibar na Udiwani katika kata 12 za Tanzania
Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 Desemba mwaka 2022.