Wasimamizi wa Vituo vya Kupigia Kura Kata ya Kinyika watakiwa kuepuka kuvuruga uchaguzi
Imewekwa: July 10, 2023
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Makete Bw. William Makufwe amewataka wasimamizi wa vituo vya kupigia kura katika Kata ya Kinyika kuelewa mafunzo na kuyazingatia watakayofundishwa bila ya kukosea ili kuepuka kuvuruga Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata hiyo unaofanyika Julai 13, 2023.
Bw. Makufwe ameyasema hayo wakati
wa kufungua mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa
vituo vya kupigia kura vya Kata ya Kinyika ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi
Mdogo wa Udiwani wa kata hiyo.
Amesema kuwa wasimamizi na
wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura ndio kiina cha uchaguzi na ndio
wanaohitimisha mchakato wote wa uchaguzi siku ya kupiga kura, hivyo iwapo watafanya
ndivyo sivyo watakuwa wameharibu mchakato wote wa uchaguzi huo mdogo.
“Tumefanya mambo mengi kabla ya
siku ya leo na tutafanya mengi kabla ya siku ya uchaguzi lakini ninyi
wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura ndio mtakaohitimisha
maandalizi yote yaliyofanyika kuelekea siku ya uchaguzi” alisema Bw. Makufwe na
kuongeza kuwa:
“Kwa hiyo nyinyi msipoelewa
mafunzo haya, mkikosea au mkifanya ndivyo sivyo katika kutekeleza majukumu yenu
na uchaguzi ukavurugika maana yake maandalizi yote tuliyoyafanya yanakuwa
hayana maana yoyote.”
Alisema wanachotakiwa kufanya ni
kuwa wasikivu, wadadisi na wazingatie
mafunzo watakayopewa ili kutekeleza kwa usahihi yale wanayotakiwa kufanywa siku
ya uchaguzi.
Mbali na hilo, Bw. Makufwe
aliwataka wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura katika
Kata ya Kinyika kuwahudumia wapiga kura kwenye vituo kwa weledi, uadilifu na
kutumia kauli nzuri ili kufanikisha uchaguzi huo.
Aliwataka wasimamizi hao kuepuka
makosa katika kutekeleza majukumu yao na hakikisha kila mmoja anatekeleza
majukumu yake kwa usahihi kwani kuharibika kwa mchakato wa uchaguzi siku ya kuoiga
kura kutasababisha kushindwa kutoa matokeo.
Hivyo aliwataka kuzingatia maadili
ya kazi yao na wasichukulie wepesi majukumu yao kwa uzoefu walionao bali kwa
kuzingatia mambo watakayofundishwa katika mafunzo hayo.
Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika Kata ya Kinyika unafanyika kutokana na kufariki kwa diwani wa kata hiyo na kata hiyo inaungana na kata nyingine 12 zinazofanya uchaguzi huu mdogo unaotarajiwa kufanyika Siku ya Alhamisi tarehe 13 Julai, 2023.