Wasimamizi wa Uchaguzi waaswa kutofanya kazi kwa mazoea.
Imewekwa: November 17, 2022Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutoka katika Kata zinazotaraji kufanya uchaguzi mdogo wa udiwani Desemba 17, 2022 kutofanya kazi ya uchaguzi kwa mazoea, badala yake wazingatie sheria, kanuni za uchaguzi pamoja na maelekezo ya Tume katika utendaji wao.
Tume pia imewataka wasimamizi wa nchaguzi na wasimamizi
wasaidizi wa uchaguzi kuhakikisha wanavishirikisha Vyama vyote vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi ili
kurahisha utekelezaji wa majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Mhe. Magdalena Rwebangira wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya
wasimamizi wa Uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Kata
yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Mhe.Rwebangira amesema Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha,
hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa kwani hatua na taratibu
hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama
siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
“Nachukua nafasi hii kuwaasa kuwa pamoja na uzoefu ambao
baadhi yenu mnao katika uendeshaji wa
uchaguzi, ni vyema mhakikishe mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume
badala ya kufanya kazi kwa mazoea”,alisema Mhe. Rwebangira.
Aidha amewataka kujiamini na kufanya kazi kwa weledi, na
kwamba katika utendaji wa majukumu yao wanapaswa kuzingatia Katiba ya Nchi,
Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo mbalimbali
yanayotolewa na Tume na kuongeza kua jambo hilo lisiishie katika mafunzo na
nadharia bali ionekane kufuatiwa katika kutenda.
“Sanjari na hilo nawaasa kukumbuka kuvishirikisha Vyama
vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika
maeneo yenu katika masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa
kwani jambo hilo litawarahisishia sana
utekelezaji wa majukumu yenu,”alisema Mhe.Rwebangira.
Wasimamizi hao wametakiwa kuhakikisha wanayatambua na
kuyajua vizuri maeneo ambayo chaguzi
utaendeshwa ikiwemo hali ya miundombinu ya kufika katika Kata na hasa Vituo vya
kupigia kura.
“Mfanye utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili
kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu
uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani,”alisema Mhe. Rwebangira.
Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.Magdalena
Rwebangira pia amewataka wasimamizi hao kuhakikisha kuwa wanaajiri watendaji wa
vituo wenye weledi, wanaojitambua na kwa kadri inavyowezekana kuacha undugu au
upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.
Alisema jambo muhimu wanalotakiwa kuzingatia Wasimamizi
hao wa uchaguzi ni kujiamini, kufanya kazi kwa weredi na kuzingatia Katiba ya
nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, maadili ya uchaguzi pamoja na
maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume.
Aidha Mjumbe wa Tume hiyo ya uchaguzi, aliwasisitizia
wasimamizi hao wa uchaguzi kuhakikisha wanafanya utambuzi wa vituo vya uchaguzi
mapema kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi
kufanyika kwa utulivu na amani.
Naye Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
Bw. Stephen Elisante, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi alisema
uchaguzi huo mdogo wa udiwani utafanyika
katika Kata 12 za Tanzania Bara ila waliopo katika mafunzo hayo Mkoani
Morogoro ni kutoka katika Kata sita za Vibaoni – Halmashauri ya Mji wa Handeni,
Lukozi – Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Misugusugu – Halmashauri ya Mji wa
Kibaha, Majohe - Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mnyanjani - Halmashauri
ya Jiji la Tanga na Dunda - Halmashauri
ya Wilaya ya Bagamoyo.
Mapema kabla ya ufunguzi wa Mafunzo hayo watendaji w uchaguzi hao walikula kiapo cha kutunza siri na kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vyao vya siasa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro, Mhe. Japhet Bwire Manyama.