Wapiga Kura 114,647 walioandikishwa kushiriki Uchaguzi Mdogo Jimbo la Amani na Kata Saba
Imewekwa: December 16, 2022Wapiga Kura 114,647 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani Mkoa wa Mjini, Zanzibar na Kata saba za Tanzania Bara tarehe 17 Desemba, 2022.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele katika Risala ya
Uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 17 Desemba, 2022 na
kusema kuwa vituo vituo 289 vya kupigia kura vitatumika.
“Tume imekamilisha maandalizi
muhimu ikiwemo usambazaji wa vifaa vya uchaguzi na mafunzo kwa watendaji wa
uchaguzi katika ngazi ya vituo vya kupigia kura” alisema Jaji wa Rufaa
Mwambegele.
Jaji wa Rufaa Mwambelegele amesema
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wasimamizi wa uchaguzi, vyama vya siasa na
wagombea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi wakati wa Uchaguzi
Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani, Mkoa wa Mjini, Zanzibar na Uchaguzi wa
Udiwani katika Kata saba za Tanzania Bara.
Mbali na jimbo la Amani pia
uchaguzi huo mdogo utashirikisha, Kata za Majohe (Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam), Mndumbwe (Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba), Njombe Mjini
(Halmashauri ya Mji wa Njombe), Dunda (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo),
Mwamalili (Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga), Mnyanjani (Halmashauri ya
Jiji la Tanga) na Vibaoni (Halmashauri ya Wilaya ya Handeni).
Aidha, amevitaka vyama vya siasa,
wagombea na wadau wa uchaguzi kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria
vya uvunjifu wa amani kwani jukumu la kulinda amani ni la kila mwananchi, hivyo
wahakikishe wanalinda amani iliyopo sasa kwenye jimbo na kata zinazofanya
uchaguzi huo.
Jaji wa Rufaa Mwambegele amesema
Sheria na Kanuni za Uchaguzi zimeweka mamlaka na taratibu zinazotakiwa kufuatwa
iwapo kutakuwepo na malalamiko yoyote wakati wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama
vya siasa na wagombea kufuata taratibu hizo ili kuuufanya uchaguzi huo ufanyike
kwa uhuru na haki.
Mweyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi amewataka wapiga kura wote waliojiandikisha katika jimbo ya Amani na
Kata saba za Tanzania Bara kujitokeza kupiga kura ili waweze kuwachagua Mbunge
na madiwani wanaowataka.
Amevitaka vyama vya siasa wagombea
na wafuasi wao kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi zimekamilika tarehe 16
Desemba, 2022 saa 12:00 jioni hivyo hawaruhusiwi kufanya mikutano ya kampeni
kuanzia muda huo na hawaruhusiwi kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni
kama vile vipeperushi, bendera na mavazi.
Aidha Jaji Rufaa Mwambegele
amevikumbusha vyama vya Siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi wa huo, kuzingatia
wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia, kuhesabu na
kujumlishia kura.
“Pili upigaji kura utafanyika
katika vituo vya kupigia kura vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2020.Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa
saa 10:00 jioni.Iwapo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao walifika kabla
ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura, mtu yeyote
hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00
jioni”alisema Jaji Rufaa Mwambegele na kuongeza:
“Watakaoruhusiwa kupiga kura katika
uchaguzi mdogo wa Jimbo la Amani Wilaya ya Mjini Zanzibar ni wale tu
walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC) na wana kadi za mpiga kura” alisema Jaji wa Rufaa Mwambegele.
Aidha Jaji wa Rufaa Mwambegele
alisema “Kwa upande wa uchaguzi mdogo wa madiwani watakaoruhusiwa kupiga kura
ni wale walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Taifa
ya Uchaguzi na wana kadi zao za mpiga kura. Hata hivyo, Tume kwa
kuzingatia masharti ya kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura
343 pamoja na kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Sura 292, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika
kutumia vitambulisho mbadala”.
Amevitaja vitambulisho mbadala kuwa
ni Passi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia
kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Mpiga kura
aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika ataruhusiwa kutumia kitambulisho
mbadala iwapo tu atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
na jina lake lipo kwenye orodha ya wapiga kura anapokwenda kupiga kura. Aidha
majina yake yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yafanane na yale
yaliyopo katika kitambulisho mbadala.
Jaji wa Rufaa Mwambegele
amekumbusha kuwa katika vituo vya kupigia kura kipaumbele kitatolewa kwa
wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha
watakaokuwa na watoto vituoni na kutakuwa na majalada ya nuktanundu katika
vituo vya kupigia kura kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kuona ili weweze
kupiga kura wenyewe.
Alifafanua kuwa kwa wapiga kura
wenye ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada hayo wanaruhusiwa kwenda
vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.
Amewakumbusha wapiga kura
kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2020 yaliyokubaliwa na wahusika wote
vikiwemo vyama vya siasa, kuwa wapiga kura watatakiwa kuondoka vituoni mara tu
baada ya kupiga kura, hivyo Tume imewashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko
katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.
Jumla ya vyama vya siasa 16
vimesimamisha wagombea katika uchaguzi huo mdogo ambapo Tume imevipongeza vyama
hivyo na wagombea wao kwa kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba kujitokeza
kushiriki katika uchaguzi huu mdogo wa Ubunge na Udiwani.