Wadau wa Uchaguzi watakiwa kuwahamasisha wanachi kata ya ikoma wilayani Rorya kushiriki uboreshaji
Imewekwa: November 20, 2023
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wadau wa uchaguzi kufikisha ujumbe sahihi kwa wananchi wa Kata ya Ikoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ili wananchi wenye sifa ya kuandikishwa na kuboresha taarifa zao wajitokeze kwa wingi kushiriki uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwabainisha waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Ramadhani
Kailima wakati akifungua mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi uliofanyika
kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mapsap Linme iliyopo wilayani Rorya Mkoa wa Mara.
Aliwaasa
wadau wote wa uchaguzi kuendelea kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na
miongozo katika kipindi chote cha uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura.
“Ni
tegemeo la Tume kuona mnafikisha ujumbe sahihi kwa wananchi ambako uboreshaji
wa majaribio yatafanyika ili wananchi
wenye sifa ya kuandikishwa na kuboresha taarifa zao wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hili na
kuwabainisha waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura.
Pia,
nawaasa wadau wote kuendelea kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo
katika kipindi chote cha uboreshaji wa majaribio la Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura.”, alisema Bw. Kailima.
Mbali
na kuwaasa wadau hao wa uchaguzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi alisema kuwa Tume imejipanga
kuhakikisha kuwa wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu uboreshaji wa
majaribio kwa kutumia njia mbalimbali za kutoa elimu ya mpiga kura zikiwemo;
kukutana na wadau wengine wa uchaguzi.
Aliongeza kuwa vyama vya siasa
vitashiriki katika uboreshaji wa majariobio kwa kuweka wakala mmoja katika kila
kituo cha kuandikisha wapiga kura, lengo ni kushuhudia na kujiridhisha juu ya
taratibu zitakazotumika wakati wa uboreshaji wa majaribio wa Daftari.
Alisisiti kwa kuwaomba wadau
wa uchaguzi kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na mapendekezo kwenye
mkutano huo ili kufanikisha utekelezaji wa uboreshaji huo.
Mkutano huo wa wadau wa
uchaguzi umewashirikisha viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wazee
wa kimila, watu wenye ulemavu, wawakilisha wa vijana, wawakilishi wa wanawake
na asasi za kiraia kwa ujumla kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
itafanya uboreshaji wa majaribio
wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata ya Ikoma iliyopo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa huu wa Mara na Kata ya Ng’ambo iliyopo
katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, mkoa wa Tabora, utakaofanyika kuanzia
tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.