Vyama vitano vyachukua fomu za uteuzi Uchaguzi Mdogo Jimbo la Mbarali
Imewekwa: August 14, 2023Vyama vitano vya Siasa vimechukua fomu za uteuzi wa wagombea Ubunge katika Jimbo la Mbarali Mkoa wa Mbeya kuwania kiti hicho katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge unaotarajiwa kufanyika tarehe 19 Septemba mwaka 2023.
Vyama
vilivyochukua fomu ni Chama cha AAFP kikiwakilishwa na Bi. Halima Abdalah
Magomba, Chama cha DP kupitia kwa Bw. Osward Joseph Mndeva, Chama cha UDP
kikiwakilishwa na Bw. Zavely Laurent Seleleka, Chama cha CCK kilichomtea Bw. Exavery
Town Mwataga kuwa mgombea wake na Chama cha UPDP kikiwalishwa na Bw. Bosco
Daudi Mahenge.
Wagombea wa
vyama hivyo wamekabidhiwa fomu za uteuzi na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la
Mbarali Bw. Missama Kwangura katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi zilizopo
Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.
Akizungumza
wakati wa kukabidhi fomu hizo, Bw. Kwangura aliwakumbusha wagombea wa vyama
hivyo kujaza fumo hizo kwa usahihi ikiwemo wadhamini wasiopungua 25
walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Jimbo la Mbarali.
“Kwa
kuzingatia taratibu za uteuzi baada ya kujaza fomu hizi mnaweza kuzileta siku
tatu kabla ya siku ya uteuzi ili tuweze kuzihakiki na kufanya marekebisho pale
ambako kuna mapungufu katika kujaza fomu hizi” alisema Bw. Kwangura.
Aliwapongeza
wagombea hao kwa kuonesha nia ya kugombea kiti cha Ubunge katika jimbo hilo
kwani hatua hiyo inaimarisha demikrasia katika uchaguzi nchini.
Utoaji fomu
za uteuzi kwa wagombea umeanza jana tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023 ambayo
itakua siku ya uteuzi wa wagombea katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Mbarali
na Udiwani katika Kata Sita za Tanzania Bara.
Kwa mujibu
wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 20
Agosti hadi tarehe 18 Septemba na tarehe 19 Septemba, 2023 itakuwa siku ya
kupiga kura.