Tume yawataka wasimamizi wa uchaguzi kuvishirikisha vyama vya siasa wakati wa uchaguzi
Imewekwa: June 19, 2023
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka Masimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata kuvishirikisha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Hayo yamesema na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji
Mst. Thomas Mihayo wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi hao wa uchaguzi
yanayofanyika Mjini Iringa, ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mdogo wa Madiwani
katika kata 14 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 13 Julai mwaka
2023.
Alisema iwapo kuna mambo hayahitaji kuwashirikisha wadau hao
wasiwashirikishe na wala wasishinikizwe kuwashirikisha na kama yapo mambo
ambayo wanapaswa kuwashirikisha basi ni lazima wawashirikishe ili kurahisisha
majukumu yao.
Jaji Mst. Mihayo aliongeza kwa kuwataka wasimamizi hao wa
uchaguzi kufuata na kuzingatia hatua na taratibu za kisheria katika kutekeleza
majukumu yao kwani hatua na taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri na
wenye ufanisi na hupunguza malalamiko katika uchaguzi.
“Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu
mbalimbali za kisheria ambazo hupaswa kufuatwa na kuzingatiwa kwani hatua na
taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo
kupunguza kama si kuondoa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa
uchaguzi”, alisema Jaji Mst. Mihayo na kuongeza:
“Jambo muhimu mnalotakiwa kuzingatia ni kujiamini na kufanya
kazi kwa weledi na kwamba katika utendaji wa majukumu yenu, mnapaswa kuzingatia
Katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na
maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki
cha uchaguzi mdogo”.
Aliwasisitiza wasimamizi hao wa uchaguzi kuzingatia masuala
muhimu ikiwa ni pamoja na kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili
kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio
mzuri unaoruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
Jaji Mst. Mihayo aliwataka wasimamizi hao kuhakikisha wanaajiri
watendaji wa vituo wenye weledi, wanaojitambua na kwa kadri inavyowezekana
waachane na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli
za uchaguzi.
“Kuhakikisha vifaa vya uchaguzi mnavyovipokea kutoka Tume na
kuhakikisha kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema. Kuhakikisha siku ya
uchaguzi mnaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kinafunguliwa
saa 1:00 asubuhi na kufanya mawasiliano na Tume pale ambapo utahitajika ushauri
kuhusiana na masuala ya uchaguzi uliopo.”, alisema Jaji Mst. Mihayo.
Mafunzo haya ya siku tatu kwa Masimamizi wa Uchaguzi na
Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi lengo lake ni kuwajengea uwezo na kuwakumbusha
wajibu na majukumu yao wakati wote wa uchaguzi na yanafanyika pia katika mkoa
wa Tanga kwa watendaji wengine wanaotarajia kusimamia uchaguzi mdogo kutoka
katika halmashauri nyingine.