Tume yawataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanasimamia uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika
Imewekwa: June 21, 2023
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wasimamizi wa uchaguzi wa kata zinazofanya uchaguzi mdogo wa madiwani kuhakikisha wanaongozwa na Katiba, Sheria za Uchaguzi na Maelekezo ya Tume katika kutekeleza majukumu yao ili kusimamia uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji
Mst. Thomas Mihayo wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wa
uchagizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata
yaliyofanyika mjini Iringa.
Alisema shughuli zote za uchaguzi zonaongozwa na Katiba,
Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo ya Tume, hivyo Tume
inawasisitiza washiriki kusoma miongozo hiyo wakati wote wanapotekeleza
majukumu yao.
Jaji Mst. Mihayo pia aliwataka wasimamizi hao wa uchaguzi kutekeleza
majukumu yao kwa ufanisi na weledi kwa kuzingatia ratiba ya utekelezaji ili
kufanikisha uchaguzi huo utakaofanyika Julai 13, 2023 katika kata 14 za
Tanzania Bara.
Aliongeza kuwa jukumu lililo mbele yao ni kubwa na linahitaji
umakini na kujitoa, hivyo wazingatie umahiri, umakini na weledi katika kutekeleza
jukumu hilo ikiwemo kuwapata watendaji wa vituo wenye sifa na uwezo wa kufanya
kazi hiyo muhimu.
“Ni matarajio ya Tume kwamba baada ya kupatiwa mafunzo haya,
mtatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na weledi mkizingatia ratiba ya utekelezaji
ili kufanikisha uchaguzi wa terehe 13 Julai, 2023” alisema.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi
Jimbo la Kilosa Kisena Mabuba aliishukuru Tume kwa kupata mafunzo hayo na
kuahidi kwa niaba ya wenzake kwenda kusimamia sheria na taratibu za uchaguzi
ili uchaguzi uende kwa amani.