Tume yawataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao wajitokeze kujiandikisha na kuboresha taarifa zao
Imewekwa: June 17, 2019
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao juu ya kushiriki kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura au kuboresha taarifa zao ili kila mwananchi mwenye sifa za kuandkishwa akaandikishwe na yule anayeboresha taarifa zake akaboreshe.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Jaji Semistocles Kaijage wakati akifungua mkutano wa Tume na viongozi wa dini
jijini Dar es Salaam leo, ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la
Wapiga Kura ambayo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Jaji Kaijage amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatambua
umuhimu wa viongozi wa dini na iwapo viongozi hao wakielewa vyema mchakato wa
uandikishaji na uchaguzi kwa ujumla watawawezesha wananchi kushiriki katika
mchakato wa uchaguzi kwa amani kwani wanaongoza kundi kubwa la wananchi na
wanao ushawishi mkubwa kwa waumini wao.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amesema taasisi
yake inatambua umuhimu wa viongozi wa dini na imekuwa ikiwatumia viongozi hao kuhamasisha
ushiriki katika chaguzi kwa amani na kutokana na juhudi za viongozi hao,
chaguzi hizo zimekuwa zikifanyika kwa amani na utulivu.
Akijibu baadhi ya maswali ya viongozi hao wa dini, Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia amesisitiza kuwa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi itandelea kutenda haki katika kusimamia chaguzi na
kuendelea kukutana na wadau wa uchaguzi na kuwapa elimu ili kupunguza
malalamiko yanayotolewa katika chaguzi.
Dkt. Kihamia amewaeleza viongozi wa dini kuwa kwa sasa malalamiko katika chaguzi mbalimbali
yamepungua kwa kiwango kikubwa na amewahakikishia kuwa yataendele kupungua.
Wakizungumza kwenye mkutano huo, baadhi ya viongozi wa dini
wameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwashirikisha katika mkutano huo
kwani wanaamini viongozi wa dini wakishirikishwa ipasavyo kwenye mchakato wa
uchaguzi, chaguzi zitaendelea kufanyika kwa amani na mafanikio.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kukutana na wadau wa
uchaguzi ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura
unaotarajiwa kuanza Julai mwkaa huu ambapo Jumanne ya wiki itakutana na
wawakilishi wa taasisi za wanawake.