Tume yatoa vibali kwa Asasi tatu kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi wa Udiwani wa Desemba 17, 2022
Imewekwa: December 01, 2022
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa vibali vya kutoa Elimu ya Mpiga Kura kwa Taasisi au Asasi tatu za Kiraia kwenye Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika Kata tatu za Tanzania Bara.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Nassoro
Shemzigwa vibali hivyo vimetolewa baada ya kikao cha Tume kilichokaa tarehe 25
Novemba mwaka 2022.
“Baada
ya uhakika na upembuzi wa maombi yaliyopekelewa, Tume katika kikao chake cha
tarehe 25 Novemba, 2022 iliridhia Taasisi au Asasi zifuatazo kupewa vibali kwa
ajili ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura” alisema Bw. Shemzigwa.
Alizitaja
taasisi au asasi hizo kuwa ni Tanzania Building Future Organization (TABUFO) ya
Mkoa wa Mtwara iliyopewa kibali kutoa elimu katika Kata ya Mndumbwe iliyopo
Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.
Taasisi
au Asasi nyingine iliyopewa kibali ni Tanzania Peace, Legal Aid and Justice
Centre (PLAJC) ya Mkoa wa Dodoma iliyopewa kibali kutoa Elimu katika Kata ya
Dabalo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Aliongeza
kuwa Taasisi au Asasi ya Umbrella of Women and Disabled Organization (UWODO) ya
Mjini Njombe ilipewa kibali cha kutoa Elimu kwenye Kata ya Njombe Mjini katika
Halmashauri ya Mji wa Njombe.
“Tume
ya Taifa ya Uchaguzi inazikumbusha Taasisi au Asasi hizo kuwa zitawajibika
kujigharamia katika zoezi la kutoa Elimu ya Mpiga Kura” alibainisha Bw.
Shemzigwa.
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 4 C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume
imepewa mamlaka ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia
Taasisi au Asasi na watu wanaotaka kutoa elimu hiyo.
Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani Tanzania Zanzibar na Udiwani katika Kata 12 za Tanzania Bara unatarajiwa kufanyika tarehe 17 Desemba mwaka 2022.