Tume yatangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Majimbo ya Konde na Ushetu kufanyika tarehe 9 Oktoba, 2021
Imewekwa: August 27, 2021TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuwepo kwa nafasi mbili za Ubunge katika majimbo ya Konde mkoa wa Kaskazini Pemba na Ushetu mkoani Shinyanga.
Akizungumza na Vyombo vya habari leo tarehe 27 Agosti 2021, Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera amesema uchaguzi huo
mdogo wa marudio umepangwa kufanyika Oktoba 9,2021.
“Ratiba ya uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa
wa Kaskazini Pemba na Jimbo la Ushetu Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga ipo
tayari,”alisema Dkt. Mahera.
Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Kumb. Na. CEA.137/400/02/111 ya tarehe 16
Agosti 2021, akiitaarifu kuhusu kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo
la Ushetu Mkoani Shinyanga.
Nafasi hiyo inatokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Elias John
Kwandikwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dkt Mahera amesema taarifa hiyo ya Spika ni kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Aidha, kwa upande wa Jimbo la Konde, Dk Mahera amesema mnamo tarehe 2 Agosti,
2021 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa taarifa kwa umma kuhusu kuwepo wazi
kwa Jimbo la Konde lilipo katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa
Kaskazini Pemba kutokana na mbunge mteule wa jimbo
hilo, Sheha Mpemba Faki kujiuzulu.
“Tume ilipokea barua yenye Kumb. Na. CMM/T.40/Vol.I/72 ya tarehe 2 Agosti, 2021
kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikitoa taarifa kuwa Mbunge
Mteule wa Jimbo la Konde, ameandika barua, kueleza kwamba hakuwa tayari
kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Konde kutokana na changamoto za
kifamilia,”alisema Dkt. Mahera na kuongeza kuwa kutokana na hatua hiyo, Tume
ililitangaza jimbo hilo kuwa wazi kwa kuwa Mbunge huyo Mteule alikuwa bado
hajatangazwa katika Gazeti la Serikali kwa mujibu wa kifungu cha 81(c) (iii)
cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Awali mnamo tarehe 18 Julai, 2021 Tume iliendesha Uchaguzi mdogo katika Jimbo
la Konde kujaza nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa
jimbo hilo, Khatibu Saidi Haji kupitia chama cha Alliance for Change and
Transparency (ACT –WAZALENDO)
Maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo yameshafanyika na kazi ya utoaji fomu za
uchaguzi kwa wagombea inaanza Septemba 13 hadi 19,2021 huku uteuzi wa wagombea
watakao wania nafasi hizo ukifanyika Septemba 19 mwaka huu.
Aidha, Dkt Mahera amesema kampeni za uchaguzi katika majimbo hayo ya Ushetu na
Konde utaanza Septemba 20, 2021 na zitafikia ukomo wake Oktoba 8 mwaka huu na
uchaguzi kufanyika 9 Oktoba ,2021.
Dk Mahera amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavikumbusha vyama vya siasa na
wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi,
taratibu, miongozo na maelekezo yatakayotolewa na Tume katika kipindi cha
Uchaguzi mdogo.