Tume yatangaza Uchaguzi Mdogo Jimbo la Amani na Kata 12 za Tanzania Bara kufanyika Desemba 17, 2022
Imewekwa: October 30, 2022
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Amani katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Tanzania Zanzibar na Madiwani katika Kata 11 za Tanzania Bara utakaofanyika tarehe 17 Desemba mwaka 2022.
Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles, amesema katika
taarifa kuwa uchaguzi huo umetokana na vifo vya Mbunge wa Jimbo la Amani na fivo
vya madiwani na wengine kujiuzulu.
Dkt. Charles
alifafanua kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea barua kutoka kwa Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiitaarifu Tume kuwepo nafasi wazi ya
Ubunge katika Jimbo la Amani kufuatia kifo cha mbunge wa jimbo hilo Mhe. Mussa
Hassan Mussa (CCM) kilichotokea Oktoba 13, 2022.
Aliongeza
kuwa aidha Tume ilipokea barua kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akiifahamisha Tume kuwepo nafasi wazi
za udiwani katika kata 12 kwenye halmashauri 11 za Tanzania Bara kutokana na
vifo na kujiuzulu kwa madiwani.
“Kwa kuzingatia
masharti ya Kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343
na Kifungu cha 13 (2) cha Sheria ya Uchaguzi
ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume imeaandaa Uchaguzi Mdogo ili
kujaza nafasi ya Ubunge Jimbo la Amani na nafasi za Udiwani katika kata 12 za
Tanzania Bara” alisema Dkt. Charles.
Kwa mujibu wa
ratiba ya uchaguzi huo Fomu za Uteuzi zitatolewa kuanzia tarehe 24 hadi 30
Novemba, 2022, Uteuzi wa Wagombea utakuwa tarehe 30 Novemba, 2022, Kampeni za
Uchaguzi zitaanza tarehe 1 hadi 16 Desemba, 2022 na Siku ya Kupiga Kura itakuwa
tarehe 17 Desemba mwaka 2022.
Dkt. Charles
alitaja kata zitakazofanya Uchaguzi Mdogo wa Madiwani na halmashauri na mkoa
yake kwenye mabano kuwa ni Kata ya Majohe (Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam-Dar es Salaam), Kata ya Dabalo (Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino-Dodoma)
Kata ya Ibanda (Halmashauri ya Wilaya ya Kyela-Mbeya), na Kata ya Mndumbwe (Halmashauri
ya Wilaya ya Tandahimba-Mtwara).
Kata
ninyingine ni Kata ya Njombe Mjini (Halmashauri ya Mji wa Njombe-Njombe), Kata
ya Misugusugu (Halmashauri ya Mji wa Kibaha-Pwani, Kata ya Dunda (Halmashauri
ya Wilaya Bagamoyo-Pwani), Kata ya Kalumbeleza (Halamashauri ya Wialaya ya
Sumbawanga-Rukwa), Kata ya Mwamalili (Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga- Shinyanga),
Kata ya Mnyanjani (Halmashauri ya Jiji la Tanga-Tanga) Kata ya Lukozi
(Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto-Tanga) na Kata ya Vibaoni iliyopo Halmashauri
ya Mji wa Handeni Mkoa wa Tanga.