Tume yakutana na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
Imewekwa: December 14, 2017Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, amesema kuna amani na utulivu wa kutosha kwa Wananchi wa Zanzibar hasa baada ya kukamilika kwa Uchaguzi wa marejeo Visiwani humo uliofanyika Machi 20,2016.
Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ulilazimika kurejewa baada
ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa awali uliofanyika Oktoba
25,2015,kutokana na kukiukwa kwa taratibu mbalimbali zinazosimamia na kuendesha
uchaguzi na hivyo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kulazimika kufuta matokeo ya
Uchaguzi huo.
Makamu wa Pili wa Rais amesema hayo wakati akipokea
taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 25,2015
toka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian
Lubuva,Ofisini kwake Vuga,Zanzibar leo.
Katika hotuba yake Makamu wa Pili wa Rais aliwaeleza
Makamishna wa Tume kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilijitahidi kufanya
mazungumzo na upande wa upinzani kupata muafaka kuhusina na kukiukwa kwa
taratibu za Uchaguzi na nini kifanyike baada ya hapo.
Hata hivyo,tofauti na makubaliano ya mazungumzo,Katibu
Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),aliamua kufanya Mkutano na Waandishi wa habari
baada ya vikao nane na hivyo kukiuka taratibu za kuendesha mazungumzo ya vikao
hivyo.
Baada ya kukiukwa kwa taratibu hizo,serikali ilitangaza
tarehe ya kurudiwa, kwa uchaguzi na vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi wa
Oktoba 25,2015 walipaswa pia kushiriki katika uchaguzi wa marejeo ambapo chama
cha Wananchi (CUF) ,hakikushiriki katika Uchaguzi huo.
Awali kabla ya kukabidhi taarifa hiyo,Mwenyekiti wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damiani Lubuva alimweleza Makamu wa Pili
wa Rais Balozi Seif Ali Idd kuwa inaweza kuendelea mchakato wa majukumu mengine
ikiwemo maandalizi ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Wakati huohuo,Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Jaji Mstaafu Damian Lubuva alikabidhi taarifa hiyo ya Uchaguzi Mkuu kwa Spika
wa Baraza la Wawakilishi Zuber Ali Maulid katika ofisi za Bazara za Baraza
hilo.
Katika hafla hiyo,Mwenyekiti alimweleza Spika wa
Baraza la Wawakilishi kuwa ni muhimu kuimarisha uhusiano uliopo na kujenga
ushirikiano zaidi ili kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu
mbalimbali ya kila siku.
Kwa upande wake, Spika Ali alisema amefurahishwa na
ziara hiyo ya Makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwani inatoa nafasi ya
kuelewa jinsi ambavyo Baraza la Wawakilishi linatekeleza majukumu yake katika
kuwahudumia wananchi waliowachagua.
Aidha,Mkurugenzi wa uchaguzi Bwana Kailima Ramadhani
pia, alipata fursa ya kukabidhi taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Rais,Wabunge na
Madiwani kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar(ZEC) Bwana Salum Kassim Ali.
Katika ziara hiyo ya siku tatu ambayo ilikuwa ya
kawaida,Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damin Lubuva
alifuatana na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mkuu Mstaafu
wa Zanzibar Hamid M. Hamid,Wajumbe wa Tume Jaji Mstaafu John Mkwawa na Mary
H.C.S Longway,Mchanga H.Mjaka,Asina Omari na Katibu wa Tume na Mkurugenzi wa
Uchaguzi Kailima Ramadhani.
Ziara hiyo imekamilika leo, na Wajumbe hao wa Tume wanajiandaa kwa ziara
kama hiyo ambayo itafanyika mjini Dodoma kuanzia kesho tarehe 28/06/2016.