Tume yakagua eneo la ujenzi wa jengo la Ofisi Dodoma
Imewekwa: December 14, 2017
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damin Lubuva amesema Tume imeridhika na kufurahishwa na kiwanja ambacho imepatiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA),na Tume iko tayari kuanza taratibu za ujenzi katika eneo hilo.
Kiwanja hicho chenye ukubwa wa mita za eneo 36,000 sawa na ekari 10, kimeigharimu Tume ya Taifa ya Uchaguzi shilingi milioni 475 na kiko katika eneo la Ndenjengwa nje kidogo ya Manisapaa ya Dodoma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kutembelea eneo hilo, Jaji Lubuva amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inajivuna kupata eneo hilo na iko tayari kuanza ujenzi pindi taratibu zitakapokamilika na kuwa miongoni mwa Taasisi za Serikali ambazo zitahamia Dodoma.
Naye Mkurugenzi wa UIchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bwana Kailima Ramadhani, akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa,ufanisi katika utendaji wa Shughuli za Tume utaimarika baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Jengo la Tume kutokana na ukweli kuwa utekelezaji wa majukumu ufanyika katika jengo moja.
Kwa sasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatumia majengo ambayo yako sehemu tatu tofauti na kusababisha utendaji kuwa katika mazingira magumu ya utekelezaji wa majukumu. 2 Aidha,bwana Ramadhani amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo,watumishi watafanya kazi katika mazingira salama na tulivu ikilinganishwa na sasa ambapo Tume inatumia ofisi za kupanga ambazo pia zinatumiwa na wapangaji wengine.
Bwana Ramadhani amebainisha pia kuwa taratibu za maandalizi ya ujenzi wa jengo ziko mbioni ikiwemo kuandaa michoro ya jengo na kukamilisha taratibu nyingine za kuwapata wazabuni kwa ajili ya kufanya kazi ya ujenzi.
Kwa upande wake,Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA),Bwana Elius Mwakalinga amesema TBA iko tayari kutoa ushauri wa kujenga jengo bora pindi taratibu za michoro zitakapokamilika.
Bwana Mwakalinga amesema TBA iko tayari kushirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuhakikisha kuwa ujenzi wa jengo hilo unafanyika kwa kuzingatia taratibu na kuzingatia teknolojia ya kisasa kulinga na eneo ambalo jengo hilo litajengwa ili kukidhi mahitaji.
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,wako katika ziara ya siku nne Mkoani Dodoma ambapo pamoja na kutembelea eneo la Kiwanja kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi za Tume,kesho 30/06/2016 wanatarajiwa kutembelea Ofisi za Bunge na Kuonana na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa