Tume ipimwe kutokana na utendaji kazi wake - Jaji Lubuva
Imewekwa: August 28, 2017
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika banda la Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kwenye viwanja vya SabaSaba jijini Dar es Salaam amesema, licha ya
kuwa Mwenyekiti na Wajumbe wengine wa Tume wanateuliwa na Rais, Tume imekuwa
ikifanya kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu yeyote, taasisi, au hata
viongozi walioko madarakani.
Jaji Lubuva amesema kuwa uhuru wa Tume ambao Wananchi wengi wamekuwa
wakiuzungumzia ni fikra tu za mtu anavyodhani juu ya namna Tume iundwe na si
utendaji halisi wa Tume namna inavyotekeleza majukumu yake.
Ili kuondoa dhana hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imependekeza katika
katiba inayopendekezwa kuwa mfumo wa kuwapata Wajumbe wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ufanyiwe marekebisho ili kuwapata wajumbe kwa njia tofauti na ilivyo
sasa.
Hata hivyo Jaji Lubuva ameshauri kuwa, Wajumbe wanaounda Tume ya Taifa ya
Uchaguzi wasitokane na itikadi za vyama vya siasa ili kuepusha mgongano wa
kimaslahi ambao unaweza kujitokeza katika utekelezaji wa majukumu hasa wakati
wa kufanya maamuzi.
Akitolea mfano Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya, iliundwa kutokana na
mapendekezo ya katiba mpya na kuitwa kuwa ni Tume huru lakini hivi sasa wale
ambao hawakushinda katika Uchaguzi uliosimamiwa na Tume hiyo wameeleza kuwa
Tume ya sasa ni mbaya zaidi kuliko iliyokuwepo hapo awali.
Mwenyekiti Lubuva ametoa wito kwa Wananchi wa Tanzania kuwa wasifikiri kuwa
jina la Tume kuitwa huru ndio linaifanya Tume kuwa huru, bali uhuru wa Tume
unatokana na utendaji kazi wake bila kuingiliwa na mtu, taasisi, au kiongozi
yeyote aliyeko madarakani.
Jaji Lubuva ametembelea mabanda mbalimbali katika maonyesho ya SabaSaba yanayoendelea likiwemo banda la Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jeshi la kujenga Taifa, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama Kuu na Pride Tanzania.