NEC YACHANGIA DAMU HOSPITALI YA UHURU DODOMA.
Imewekwa: June 21, 2022Katika kuadhimisha wiki ya utumishi wa umma nchini ambayo kila mwaka hufanyika kuanzia tarehe 16 -23 Juni, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuchangia damu na kufanya usafi katika Hospitali ya Uhuru iliyopo katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Watumishi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi wameshiriki utoaji
wa damu ikiwa ni kuunga mkono jitihada za kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa,
wakina mama wajawazito na watoto.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo,
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Chamwino Dkt. Abdul Pumzi amesema uhitaji wa damu
katika hospitali zetu nchini ni mkubwa mno, hivyo amewapongeza watumishi kutoka
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kujitoa kwao kwa kuchangia damu kama sehemu ya maadhimisho
ya wiki ya Utumishi wa Umma.
“Ni furaha kuwaona
watumishi wa umma kama nyinyi mkishirki na kuunga mkono uchangiaji wa damu. Tumekuwa
tukizunguka mijini na vijijini kuhimiza uchangiaji wa damu na hii ni kutokana na
uhitaji wake kuwa mkubwa sana kwenye hospitali zetu. Kuna wa kina mama
wajawazito, kuna majeruhi wa ajali mbalimbali,
kuna watoto, wote hawa wana uhitaji wa damu,
hivyo kuja kwenu hapa ni ishara ya moyo wa upendo” alisema Dkt.Pumzi.
Awali akizungumza na Watumishi wa Tume, Muuguzi Mfawidhi wa
Hospitali hiyo ya Uhuru Bi. Joyce Nchimbi aliupongeza uongozi wa Tume kwa kuwafikiria
na kufika katika hospitali hiyo na kushiriki zoezi la usafi na uchangiaji wa damu
kama sehemu ya kuadhimisha kuadhimisha wiki ya utumishi wa Umma. Alitoa wito kwa
taasisi na mashirika binafsi kujitoa kwa namna hiyo ili kuokoa maisha ya wagonjwa
walio wengi katika hospitali zetu nchini.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa RasilimaliWatu kutoka Tume ya
Taifa ya Uchaguzi Bw. Leonard Tumua amesema ushiriki wa watumishi katika uchangiaji
wa damu na ufanyaji wa usafi katika wiki hii ya utumishi wa Umma unalenga kujenga
mahusiano mema kati ya wadau ambao ni wananchi na Tume ya Taifa ya uchaguzi.
“Sisi kama Tume tunafanya kazi na wadau mbalimbali, hivyo
kushiriki katika mazoezi kama haya, kunatuweka karibu na wadau wetu ambao ni wananchi,
kunadumisha mahusiano mema na upendo miongoni
mwetu sote” Alisema Bw.Tumua.
Nao baadhi ya watumishi
kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi walioshiriki zoezi hilo wamesema,
wamefurahishwa na uongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwaruhusu kushiriki
zoezi la ufanyaji wa usafi lakini pia kutoa damu ikiwa ni
ishara ya upendo wa watanzania waliopo hospitali na wenye uhitaji wa Damu.
“Tunashukuru sana uongozi wetu ukiongozwa na Dkt. Wilson Mahera
Charles kwa kuona umuhimu wetu kama watumishi kushiriki katika shughuli za kijamii
hasa uchangiaji wa Damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa.” alisema Bw. ErastoMwakalinga.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma imeanza Tarehe 16 mwezi Juni na inatarajia kumalizika Tarehe 23 mwezi Juni 2022 huku ikiwa na ujumbe “Nafasi ya Mapinduzi ya nne ya Viwanda katika masuala mapya yanayojitokeza kuhusu utoaji wa huduma na urejeshaji wakati na baada ya janga la Corona”.