Tume yaongeza siku tatu kwa wasimamizi wa uchaguzi kuapisha mawakala wa vyama vya siasa kwa ajili ya uchaguzi
Imewekwa: October 23, 2020
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeongeza siku tatu kwa wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo yote nchini kuapisha mawakala wa vyama vya saisa kwa ajili ya siku ya uchaguzi tarehe 28 Oktoba, 2020.
Uamuzi huo
umetangazwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo Dkt. Wilson Mahera Charles
wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Dkt. Charles
amesema siku hizo tatu ni kuanzia tarehe
21 hadi 23 Oktoba, 2020 na uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao cha Tume
kilichokaa siku ya jumatano tarehe 21 Oktoba, 2020.
Amesema Tume
imefanya uamuzi huo kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa na Kifungu cha 57 (2) cha
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ikisomwa pamoja na Kifungu cha 58 cha
Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.
Ameongeza
kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na changamoto ya kutofikika
kwa urahisi kutokana na jiografia na hivyo kuwa vigumu kwa wasimamizi wa
uchaguzi kuwafikia na kuwaapisha mawakala hao kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo,
Dkt. Charles alivitaka vyama vya saisa vipeleke orodha ya mawakala wao na viwe
vimewapanga mawakala hao katika vituo vya kupigia kura na kuweka anuani au
namba ya simu ya kila wakala husika.
“Lakini
tunaviasa vyama vya saisa kupeleka mawakala kwa utaratibu unaokubalika na iwapo
vitapeleka mawakala wasiohusika au kuwapeleka kwenye eneo ambalo sio lao na
bila kufuata utaratibu wanaweza kujikuta wako matatani”, amesema Dkt. Charles
na kuongeza:
“Ila ni
matarajio ya Tume kuwa hii kazi ya kuwaapisha mawakala wa vyama vya siasa
litaendelea kufanyika kwa utaratibu mzuri ambapo wasimamizi wa uchaguzi
watatenga maeneo katika jimbo ambayo yanafikika kiurahisi”
Dkt. Charles
amevitaka vyam vya siasa kufuata utaratibu wa kisheria na kwa mujibu wa
maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea vitapata fursa kwa mawakala wao
kuapishwa.
Amefafanua
kuwa mawakala wa vyama 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu wanatarajiwa
kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na Urais.