Tume yamtangaza Dkt. Magufuli kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Oktoba 28, 2020
Imewekwa: October 31, 2020Tume ya Taifa ya Uchaguzi imemtangaza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupata kura nyingi halali kuliko wagombea wengine na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM katika Uchaguzi wa Rais uliofanyika tarehe 28 Oktoba mwaka huu.
Hayo
yametangazwa jijini Dar es Salaam tarehe 30 Oktoba, 2020 na Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Rufaa Mst. Semistocles Kaijage baada ya kukamilika
kwa utangazaji wa matokeo ya kura za Rais katika majimbo yote 264.
Jaji Kaijage
amesema mgombea huyo wa CCM amepata kura 12,516,252 kati ya kura halali
14,830,195 zilizopigwa na idadi halisi ya waliopiga kura 15,091,950 kati ya
wapiga kura 29,754,699 walioandikishwa
kwenye Daftari la Kudumu la Wapig Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na walioandikishwa kwenye Daftaria la
Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Amewataja
wagombea wengine kutoka vyama 14 vilivyoshiriki katika uchaguzi wa Rais na kura
walizopata kwenye mabano kuwa ni Mahona Leopold Lucas wa NRA (80,787), Shibuda John Paul wa chama ADA TADEA (33,086)
na Muttamwega Bhatt Mgaywa wa chama cha SAU (14,922).
Amewataja
wagombea wengine ni Cecilia Augustino Mmanga wa Chama cha Demokrasia Makini aliyepata
kura 14, 556, Maganja Yeremia Kulwa wa
Chama cha NCCR Mageuzi amepata kura 19,969, Lipumba Ibrahim Haruna wa Chama cha
CUF amepata kura 72,885.
Jaji Kaijage
ameongeza kuwa mgombea Philipo John Fumbo kutoka Chama cha DP amepata kura
8,283, Membe Bernard Kamillius wa Chama cha ACT-Wazalendo amepata kura 81,129,
Queen Cuthbert Sendiga wa Chama cha ADC
amepata kura 7,627.
“Mgombea
Twalid Ibrahim Kadege wa Chama cha UPDP amepata kura 6,194, Rungwe Hashim Spunda wa Chama cha CHAUMA
amepata kura 32,878, Mazrui Khalfani Mohamed wa Chama cha UMD amepata kura
3,721, Seif Maalim Seif wa Chama cha
AAFP amepata kura 4,635 na Lissu Tundu Antiphas Mughwai wa Chama cha CHADEMA
amepata kura 1,933,271”, amesema Jaji Kaijage.
Baada ya
kutangaza matokeo hayo mawakala 12 wa vyama vya siasa kati ya mawakala wa vyama
vilivyoshiriki katika uchaguzi wa Rais walisaini Fomu Namba 27, kati ya
mawakala 13 waliokuwepo wakati wa kutangazwa matokeo hayo.
Jaji Kaijage
amesema ametangaza matokeo hayo kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 38 (1),
Ibara ya 41 (6) na Ibara ya 47 (2) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 35 (f) (8) na Kifungu cha 35 (h)
vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 ya Sheria za Tanzania.
Mbali na kura
halali zilizohesabiswa, Jaji Kaijage amesema idadi ya kura zilizokataliwa ni
kura 261,755.
Amesema baada
ya kutangaza matokeo hayo ya uchaguzi wa Rais, siku ya Jumapili Tume ya Taifa
ya Uchaguzi itatoa hati ya ushindi kwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa
Rais walioshinda.