Asasi zilizopata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura Zanzibar zakumbushwa mambo ya kuzingatia
Imewekwa: September 07, 2020Tume ya Taifa ya Uchaguzi imezitaka asasi za kiraia zilizopata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura Tanzania Zanzibar, kutumia vibali hivyo kutoa elimu hiyo badala ya kuchanganya elimu ya mpiga kura na kampeni za vyama vya siasa.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura Bi. Giveness Aswile wakati
akifungua mafunzo kwa asasi hizo kwenye ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,
visiwani Zanzibar.
Amesema elimu
ya mpiga kura kimsingi haitakiwi kuegemea upande wowote lakini wakati mwingine
asasi inaweza bila kujua ikajikuta inafanya kampeni kutokana na mazingira
inayotumia kutolea elimu hiyo.
“Inawezekana
hili likajitokeza kutokana na mazingira unayotolea elimu hiyo, kwa mfano
unatumia jengo la chama cha siasa au eneo linalofahamika na watu kuwa ni chama
fulani”, amesema Bi Aswile na kufafanua kuwa:-
Lengo la
maelezo haya ni kuwataka kuwa makini na mambo ambayo nayaweza kuleta
sintofahamu bila sababu yoyote ya msingi”
Amewataka
wawakilishi wa asasi hizo za kiraia kutotumia kwa ubia vibali walivyopewa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi na asasi nyingine yoyote ile na hasa zile ambazo
hazikupewa vibali hivyo.
Amefafanua
kuwa Tume hiyo inafahamu kuwa baadhi ya asasi zilizopewa vibali wakati wa
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, zilitumia vibali vyao kwa ubia
na asasi nyingine.
Bi. Aswile
amebainisha kuwa Tume inaendelea na itaendelea kufuatilia kwa karibu asasi
yoyote itakayobainika kukiuka maagizo na maelekezo waliyopewa, na kwamba Tume
haitasita kusitisha kibali cha asasi hizo wakati wowote.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Thabit Idarous
Faina amezikumbusha asasi hizo kuwa zinakwenda kuwapa elimu wananchi wa aina
tatu tofauti.
Amebainisha
makundi hayo kuwa ni wananchi ambao ni wanachama wa chama cha siasa, mashabiki
wa chama cha siasa na wale ambao hana chama chochote cha siasa.
“Kwa hiyo
tuwe makini sana wakati tunapokwenda kuwasilisha elimu yetu bila kuwakwaza wale
ambao wanakwenda kupata fursa hii ya elimu katika maeneo yao”, amesema Faina.
Wakati akiwasilisha
mada kwenye mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura
(Habari) Dkt. Cosmas Mwaisobwa amesema lengo la elimu ya mpiga kura ni kuongeza
idadi ya wapiga kura watakaokwenda kupiga kura.
Amekumbusha
takwimu za wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kuwa kati ya wapiga
kura milioni 23 ni wapiga kura takribani milioni 15 walijitokeza kupiga kura
ambayo ni idadi ndogo ya wapiga kura.
Hivyo
amesisitiza kuwa elimu ya mpiga kura inatakiwa itotelewe ili idadi ya wapiga
kura watakaojitokeza kupiga kura iongezeke.
Baadhi ya
washiriki wa mafunzo hayo wamezungumzia umuhimu wa elimu hiyo na kuipongeza
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kutoa mafunzo hayo.
Katibu Mkuu
wa Shirikisho la Michezo ya Viziwi, Zuberi Ally Haji amesema amefurahi kupata
mafunzo hayo kwani yatasaidia watu wenye ulemavu kuelimisha jamii ya watu wenye
ulemavu wa uziwi katika Unguja na Pemba.
Amesema baada
ya mafunzo hayo watu wenye ulemavu wa uziwi wanategemea kwamba itakapofika siku
ya uchaguzi ushiriki wa viziwi utakuwa ni mkubwa sana.