Elimu ya Mpiga Kura
Elimu ya Mpiga Kura ni elimu
ambayo hutolewa kwa wananchi wote kwa lengo la kuwawezesha kuelewa kuhusu
Sheria, Kanuni, Taratibu za mchakato mzima wa Uchaguzi, wajibu wao na umuhimu
wa kushiriki katika Uchaguzi, ni elimu isiyokuwa na hisia, ubaguzi wala itikadi
za kisiasa.
Elimu ya Mpiga Kura inalenga
kuwahamasisha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba katika kujitokeza na
kushiriki kuchagua viongozi wao watakao waongoza ili kujenga Demokrasia na
Utawala Bora nchini.
Dhana hii ya Elimu ya Mpiga Kura
inahusisha pia usambazaji wa taarifa, vielelezo na vipindi mbalimbali katika
Vyombo vya Habari ambavyo vinalenga kuwaelimisha Wananchi juu ya mchakato wa
Uchaguzi. Mchakato huu unahusisha Uandikishaji wa Wapiga Kura, Ugawaji wa
Majimbo, Uwekaji wazi Daftari, Kampeni, utaratibu wa Kupiga Kura na vituo vya
Kupiga Kura.
Elimu ya Mpiga Kura hutolewa kuhakikisha kuwa
Wapiga Kura wanahamasika na wanakuwa tayari kwa hiyari yao, kwa ufahamu wao na
kwa kujiamini kwao kushiriki katika mchakato wa Uchaguzi wakiwa na mtizamo wa
kukuza demokrasia.
Umuhimu
wa Elimu ya Mpiga Kura
Elimu ya Mpiga Kura ni nyenzo na
kielelezo muhimu katika kumuwezesha kila mwananchi kuelewa kuhusu mchakato wa
Uchaguzi na nafasi yake katika kupiga kura. Elimu hii huwajengea ufahamu/uelewa
wananchi kuhusu haki na wajibu wao kushiriki katika mchakato wa Uchaguzi wakiwa
na taarifa kamili na sahihi juu ya
michakato yote ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani
Mamlaka
ya Tume kutoa Elimu ya Mpiga Kura
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura
ya 343 kifungu cha 4C kimeipa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi mamlaka ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima, Kuratibu na
kusimamia Taasisi, Asasi na watu wanaotaka kutoa Elimu ya Mpiga Kura.
Kutokana na matakwa ya Sheria
iliyotajwa hapo juu, Tume hutoa Elimu ya Mpiga Kura pia kwa kushirikiana ha
Asasi za Kiraia katika kutoa Elimu hiyo.
Ushirikiano na
Asasi za Kiraia katika utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura
Aidha, Tume imekuwa ikishirikiana
na Asasi za kiraia katika kuelimisha umma kuhusu mchakato wa Uchaguzi kwa kutoa
Vibali kwa Asasi za kiraia kushiriki kutoa Elimu ya Mpiga Kura. Aidha, Tume ina
utaratibu wa kuzialika Asasi hizo zinazokusudia kutoa elimu hiyo ambapo
huwasilisha maombi na zana zao za Elimu ya Mpiga Kura ili:
i.
Kupitia na kuidhinisha zana na nyenzo zote za Elimu
ya Mpiga Kura zitakazotumiwa na Asasi za kiraia na wadau wote wanaojihusisha na
utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura;
ii.
Kupitia na kuidhinisha mipango (program) yote
iliyoainishwa na Wadau wa utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura;
iii.
Kufuatilia na Kuratibu mpango (program) wa utaoaji
wa Elimu ya Mpiga Kura ili kuhakikisha kwamba zinatolewa kwa umakini, usahihi
bila kupotosha Wananchi na zinawafikia walengwa wote waliokusudiwa; na
iv.
Kufanya tathmini ya zoezi zima la utoaji wa Elimu
ya Mpiga Kura kuona iwapo Elimu hiyo imetolewa ipasavyo na imewafikia walengwa.
Vigezo vinavyotumika katika kutoa
vibali ni pamoja na Asasi:-
- Kuwa na usajili kwa mujibu
wa Sheria za Tanzania;
- Kuwa imefanya kazi Tanzania
si chini ya miezi 6 toka kusajiliwa;
- Miongoni mwa Watendaji wake
wakuu, Wawili wanapaswa wawe Watanzania;
- Kuwa haina taarifa za
kuvuruga amani au kuchochea fujo; na
- Kuwa tayari kujigharamia
katika kutoa Elimu ya Mpiga Kura.
Aidha, Asasi inapowasilisha
maombi hayo inatakiwa kuambatanisha:-
- Cheti cha Usajili;
- Katiba ya Asasi;
- Majina ya Viongozi wa juu wa
Asasi;
- Anuani kamili ya makazi
(Physical Address) na Namba za simu za Ofisini na Viongozi;
- Zana za Elimu ya Mpiga Kura
(Vijarida, Vipeperushi, Mabango, Vipindi vilivyorekodiwa, T-shirt n.k.);
na
- Ratiba itakayoonyesha tarehe
na mahali watakapotoa Elimu ya Mpiga Kura katika halmashauri husika.
Tume imekuwa ikishirikiana na
Wadau mbalimbali wa Uchaguzi katika kuhakikisha kila mwananchi anapata Elimu ya
Mpiga Kura. Wadau hao ni pamoja na;
- Wapiga Kura
- Vyama vya Siasa
- Asasi za Kidini (FBOs)
- Asasi za Kiraia (CSOs)
- Vyombo vya Habari
- Wanawake
- Vijana
- Jumuiya za Watu wenye
Ulemavu
- Taasisi za Serikali
- Asasi za Kijamii (CBOs)
- Wadau wa Maendeleo
- Taasisi za Elimu
Ili Elimu ya Mpiga Kura iweze
kutolewa na kuleta mafanikio ni muhimu kufanya uchambuzi na kutambua makundi
ambayo yanalengwa kupatiwa elimu hiyo. Aidha, nyenzo na Vifaa vitakavyotumika
kufikisha ujumbe uliokusudiwa ni muhimu pia kutambuliwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
imeyagawa makundi haya maalum katika sehemu kuu nne kama ifuatavyo:
- Makundi yaliyojitenga
kutokana na sababu za kijiografia;
- Makundi yatokanayo na sababu
za kimaumbile;
- Makundi ya wasiojua kusoma
na kuandika;
- Wanawake na Vijana
Makundi
yanayotokana
na
sababu za kijiografia
na shughuli za kiuchumi
Makundi yanayotokana na sababu za
kijiografia ni pamoja na wafugaji, wawindaji na wakulima. Vilevile, makundi
haya ni ya watu ambao wanategemea kilimo, ufugaji na uwindaji.
Katika utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kwa kundi hili ni muhimu
kuzingatia misimu yao ya kilimo na ufugaji kwa kuwa ni watu wanaohama kutoka
eneo moja kwenda lingine kutegemeana na
hali ya hewa.
Makundi
yatokanayo na sababu za kimaumbile
Makundi haya ni yale
yanayojumisha watu wenye ulemavu wa namna mbali mbali kama vile wasioona, wenye
ulemavu wa kusikia, walemavu wa ngozi na wenye ulemavu wa viungo.
Makundi haya yanahitaji umakini
zaidi katika kuwahudumia kwa kuzingatia maumbile yao, mfano kutumia lughaza
alama na nukta nundu.
Makundi
ya wasiojua kusoma na kuandika
Kundi hili ni la wapiga kura
wasiojua kusoma na kuandika, ili kufikisha ujumbe katika kundi hili ni muhimu
kutumia picha na maelezo ili kuweza kuwapa ufahamu kuhusu haki na wajibu wao
kushiriki katika mchakato mzima wa Uchaguzi ili kuwa na taarifa kamili na
sahihi za michakato yote ya Uchaguzi.
Wanawake na vijana wameanishwa
kuwa ni makundi maalumu kutokana na na
baadhi ya Wanawake kunyimwa
haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi
kwa kuzuiliwa na waume zao
kutokana na mfumo dume. Aidha, Vijana
wengi wamekuwa wakizuiliwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa
Uchaguzi na kutumiwa na wanasiasa kuvuruga amani kwa masilahi ya wanasiasa,
yote hayo yamefanyika kutokana na uelewa finyu wa haki zao za msingi za
kushiriki katika Uchaguzi.
Njia
za utoaji Elimu ya Mpiga Kura
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa
ikitekeleza mkakati wa kutoa Elimu ya Mpiga Kura endelevu kwa kutumia njia
zifuatazo:
- Mikusanyiko rasmi ya watu: Tume inatumia maonyesho ya Sabasaba,
Nanenane, Mikutano ya Serikali za Mitaa (ALAT) na wiki ya Vijana kwa kutoa Elimu ya Mpiga
Kura ana kwa ana au kuwapatia
vijitabu na vipeperushi vyenye kuonyesha aina mbali mbali za michakato ya
Uchaguzi.
- Mikutano na wadau: Tume inatumia mikutano na wadau mbalimbali
katika kutoa elimu, Aidha imekuwa ikiandaa mikutano katika shule mbalimbali za sekondari kwa lengo
la kuwaelimisha wapiga kura watarajiwa kuhusu shughuli za Tume na
michakato ya Uchaguzi ili kuwahamasisha kushiriki katika michakato ya
Uchaguzi.
- Vipindi vya redio na Runinga: Tume inaandaa na kutekeleza programu ya
kushiriki katika vipindi mbali mbali vya redio na television ili kuweza
kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria na kanuni mbali mbali za Uchaguzi.
- Makala za magazeti: Tume inaandaa makala mbalimbali katika
magazeti mbalimbali lengo likiwa ni kutoa habari na kuelimisha umma kuhusu
Sheria na taratibu za uendeshaji Uchaguzi.
- Mitandao ya kijamii; Tume pia imekuwa ikitumia mitandao ya
kijamii katika kutoa habari za kuelimisha na kufahimisha.
- Vijitabu, vijarida na vipeperushi: Tume pia imekuwa ikiandaa
vijitabu na vijarida mbali mbali ambavyo huvigawa kwa wananchi bure lengo
likiwa ni kuwapatia uelewa kuhusu taratibu za Uchaguzi.
Katika kutoa Elimu ya Mpiga Kura
Tume hutumia zana zifuatazo:
- Vijitabu;
- Vijarida;
- Vipeperushi;
- Mabango;
- Matangazo ya Runinga na Redio na Magazeti katika kuelimisha wananchi.