Vituo vya Uandikishaji
Uandikishaji Wapiga Kura au Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la WapigaKura hufanyika kwenye vituo maalum vilivyoandaliwa kwa mujibu wa Sheria.Kifungu cha 21 kifungu kidogo cha 1 hadi cha 5 cha Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura za Mwaka 2013 kinataja vituo hivyo.
Kifungu hicho kinasema kuwa kituo cha uboreshaji kitaanzishwa angalau katika kila mtaa au kijiji ndani ya wilaya na kwenye majengo au ofisi za umma au maeneo yasiyokuwa na majengo ya umma kwa maagizo ya Mkurugenzi wa Uchaguzi kwa sharti iwe ni sehemu inayofikiwa na watu wote.
Kulingana na kifungu cha 21 (4) cha kanuni hizo za uboreshaji, vituo vya uboreshaji havitawekwa kwenye kambi za jeshi, makazi ya polisi, sehemu za ibada kama makanisa na misikiti, na kabla ya uboreshaji kuanza orodha ya vituo hivyo itakabidhiwa kwa vyama vya siasa.
Baada ya vituo kuanzishwa vitapewa namba ambazo zitatumika katika ujazaji wa fomu za uboreshaji wa daftari na anuani ya makazi ya mtu anayeomba kuandikishwa itakuwa namba maalum ya kulitambulisha eneo lake linayojulikana kama Postikodi.