Watumishi jiji la Arusha watakiwa kudumisha upendo na kufanya kazi kwa bidii
Imewekwa: January 05, 2021
Watendaji na Watumishi wa Serikali katika jiji la Arusha
wametakiwa kushirikiana,kupendana na kufanya kazi kwa bidii ili kulinda
mafanikio ya kimaendeleo yaliyofikiwa na
jiji hilo.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Arusha na aliyekuwa
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Athumani Kihamia wakati wa hafla fupi ya
makabidhiano ya Ofisi jijini hapo.
Akizungumza na Watumishi na Watendaji wa jiji hilo Dkt.
Kihamia amewataka wafanye kazi kwa bidii na kuepuka vitendo vinavyoweza kuleta
mgawanyiko miongoni mwao.
Amesema katika kipindi cha uongozi wake akiwa Mkurugenzi wa
jiji hilo aliwaunganisha watumishi wote akiweka msisitizo katika bidii, nidhamu
ya kazi na matumizi mazuri ya rasilimali na fedha Serikali hali iliyolifanya
jiji hilo kupata Hati Safi ya Matumizi ya fedha za Serikali.
“Watumishi Wenzangu mimi nimekaa katika jiji hili kwa muda
wa miaka 2, nafurahi kuwa nawaacha mkiwa na morali ya kufanya kazi na muendelee
kufanya kazi kwa bidii, mzidi kupendana ili kazi mnazozifanya zifanikiwe kwa
manufaa ya jiji ” Amesisitiza Dkt. Kihamia.
Ameongeza kuwa ili jiji hilo liendelee kupiga hatua zaidi za
Kimaendeleo, watendaji na wakuu wa Idara wana wajibu wa kufanya kazi kwa
pamoja, kuaminiana na kuepuka kufanya vitendo vya dhuruma na uonevu wa aina
yoyote kwa watumishi wa kada mbalimbali walio chini yao.
Amesema maendeleo yaliyofikiwa katika jiji hilo
yasingekuwepo kama watumishi waliopo wasingekuwa waaminifu na wanaoshauri
vizuri na kuwataka wakuu wa Idara, watendaji na watumishi wanaotoa maamuzi
kuepuka vitendo vinavyoweza kushusha chini morali ya kazi ya watumishi.
“Watendaji mlio na mamlaka msifanye mabadiliko yoyote kwa
kumwonea mtu, mafanikio haya tusingeweza kuyapata kama kusingekuwa na watumishi
wanaofanya kazi zao kwa bidii na uaminifu wapo watumishi walio na utendaji
mzuri na wanaoshauri vizuri hawa
tuendelee kuwalinda na kuwaheshimu” Amesisitiza Dkt.Kihamia.
Katika hatua nyingi Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia amesema kuwa maandalizi ya Uchaguzi mdogo wa
Ubunge na Udiwani utakaofanyika Agosti 12 mwaka huu yanaendelea na vizuri
katika maeneo mbalimbali yenye uchaguzi huo.
Amesema kuwa mpaka sasa hakuna changamoto zozote kubwa za
kiutendaji zinazoweza kukwamisha uchaguzi huo.
“ Mchakato wa uchaguzi unaenda vizuri, mpaka sasa hakuna
kasoro zozote na zoezi la Kampeni linakwenda vizuri hakuna vurugu wala vitendo
vya uvunjifu wa amani vilivyoripotiwa mpaka sasa kutokana na kampeni hizo”
Amesema Dkt. Kihamia.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa jiji hilo Mhe. Karisti
Lazaro akizungumza na Watendaji na watumishi wa jiji hilo waliohudhuria kwenye
hafla hiyo amempongeza Dkt. Athumani Kihamia kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
Ameeleza kuwa uteuzi wake umezingatia viwango vyake vya
utendaji kazi uliotukuka katika jiji hilo la Arusha uliolenga kuleta maendeleo
kwa wananchi.
“ Nichukukue fursa hii kumpongeza sana kwa namna ambavyo
Mhe. Rais amemuona katikati ya majiji yote kwa kuona anafaa kumsaidia katika
majukumu makubwa ya kitaifa”
Amewaeleza watumishi hao kwamba wana kila sababu ya
kujifunza kutoka kwa Dkt. Kihamia kwa kuwa yeye alitimiza wajibu wake kwa
uaminifu mkubwa na kuongeza kuwa kuwa
kutokana na utendaji wake jiji la Arusha liko katika hali nzuri ya mapato kwa
kuwa na asilimia zaidi ya 103, uanzishaji wa miradi mikubwa ya Afya, Elimu,
Maji na Usafirishaji ambayo yote inalenda kuinua uchumi wa jiji la Arusha.
“Hili ni fundisho kwetu, Mkurugenzi unayeondoka umetuachia
jiji letu likiwa salama, tuko kwenye mazingira mazuri sana, leo unaiacha
Halmashauri ikiwa na mapato kwa zaidi ya asilimia 103 ikiwa na Hati safi na
hoja chache sana maana ulipoingia ulikuta hoja 400 za CAG leo unaondoka ikiwa
na hoja 23 ambazo zote zinajibika, hii yote inatokana na udhibiti wake”
Amesisitiza Mhe. Lazaro.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa jiji hilo Afisa
Mtendaji wa Kata ya Ngarenaro Bw. Braison Nassari ameeleza kuwa wao kama
watumishi wa jiji hilo wanamwelezea Dkt. Athumani Kihamia kama Mkurugenzi
aliyekuwa akiwatunza watumishi wa Serikali katika jiji hilo.
Amesema kwa kipindi chote alichokuwa Mkurugenzi Dkt. Kihamia
hakukubali kuyumbishwa na mtu yeyote wakiwemo wanasiasa waliopingana naye
katika hatua zake alizozichukua katika kusimamia taratibu za Serikali na
utumishi wa umma.
“ Napenda kuweka wazi kwamba sisi kama watumishi wa jiji la
Arusha tunakupongeza sana, kwa kipindi chote ulichokuwepo hapa tuliona kwamba
hata watu walipokuwa wakileta maneno ya hila wewe ulichukua hatua ya kuchunguza
mambo hayo, na hata baadhi ya watu waliotaka kukutengenezea mambo mengi ya
kukuchafua hawakuweza kufanikiwa ulisimamia katika kulinda haki, ukweli na taratibu za utumishi “ Amesisitiza.