Wapiga kura 216,282 kupiga kura uchaguzi mdogo wa Mbarali na kata sita
Imewekwa: September 19, 2023
Wapiga kura 216,282 walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kupiga kura tarehe 19 Septemba, 2023 kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele
ameyasema hayo Wilayani Mbarali, Mkoani Mbeya leo tarehe 18 Septemba, 2023 wakati
akisoma risala kwa ajili ya uchaguzi huo na kuongeza kwamba uchaguzi utahusisha
vituo 580 vya kupigia kura.
“Katika uchaguzi
huu kuna jumla ya wapiga kura 216,282 walioandikishwa
katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao watashiriki kuchagua viongozi
wao. Aidha, uchaguzi huu utahusisha
vituo 580 vya kupigia kura vilivyobainishwa,” amesema Jaji Mwambegele.
Kata zenye uchaguzi
ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mfaranyaki iliyopo Halmashauri
ya Manispaa ya Songea, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Old
Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Marangu Kitowo iliyopo
Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya
Madaba.
Mwenyekiti wa Tume
amevikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala wa vyama, wapiga kura na
wananchi kwa ujumla kuhakikisha kwamba hawapigi kampeni siku ya kupiga kura kwa
kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
“Alama za vyama vya
siasa zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi
haviruhusiwi kutumika kesho tarehe 19 Septemba, 2023 ambayo ni siku ya uchaguzi,”
amesema.
Jaji Mwambegele
ameongeza kwamba zoezi la kupiga kura katika maeneo yote ya uchaguzi
litafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa
Mwaka 2020.
Ameongeza kwamba
vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja kamili (1:00) asubuhi na kufungwa
saa kumi kamili (10:00) jioni.
“Iwapo, wakati wa
kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa
kumi kamili (10:00) jioni katika mstari na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga
kura. Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya
saa kumi kamili (10:00) jioni,” amesema.
Jaji Mwambengele
amebainisha kwamba watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo
kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
kwenye kata husika na wana kadi zao za mpiga kura.
Ameongeza kuwa, hata
hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa, Sura ya 292 imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao
au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala.
“Mojawapo ya
kitambulisho mbadala ambacho mpiga kura anaweza kutumia ni Pasi ya Kusafiria,
Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA),” amesema.
Mwenyeki wa Tume
amesisitiza kwamba ili mpiga kura aruhusiwe kutumia kitambulisho mbadala ni
sharti awe ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake
lipo katika orodha ya wapiga kura katika kituo anachokwenda kupiga kura.
“Katika kituo cha
kupigia kura, kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee,
wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokwenda na watoto kituoni,”
amesema.
Kuhusu wapiga kura
kurudi nyumbani baada ya kupiga kura, Jaji Mwambegele amesema hilo ni sharti la
kisheria na kwamba maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa na kuridhiwa na vyama
vyote vya siasa, Serikali na Tume yanaelekeza hivyo.
Alisisitiza kwa
kusema “wapiga kura watatakiwa kuondoka kituoni mara wanapomaliza kupiga kura
ili kuepusha msongamano na vitendo vinavyoweza kuchochea uvunjifu wa
amani. Hivyo, Tume inawashauri wananchi
kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura”.
Ametoa rai kwa
wapiga kura katika Jimbo la Mbarali na kata sita zinazohusika na uchaguzi huu
mdogo, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura, ili kuwachagua
viongozi wanaowataka.
Jumla ya vyama 17 vya siasa vinashiriki kwenye uchaguzi huo mdogo, vyama hivyo vinajumuisha AAFP, ACT–WAZALENDO, ADA–TADEA, ADC, CCK, CCM, CUF, Demokrasia Makini, DP, NLD, NRA, SAU, TLP, UDP, UMD, UPDP na NCCR–MAGEUZI.