Tum yawataka mawakala na wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia sheria za Uchaguzi katika Uchaguzi Mdogo wa Mei 16, 2021
Imewekwa: May 16, 2021
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
imesema vyama vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo
ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na Uchaguzi wa Udiwani katika kata tano za
Tanzania Bara, vina wajibu wa kuweka mawakala kwenye vituo vya kupigia na
kujumlisha kura lakini mawakala hao na wasimamizi wa uchaguzi wanapaswa
kuzingatia Sheria za Uchaguzi wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Jaji wa Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage katika Risala ya Uchaguzi huo mdogo
unaotarajiwa kufanyika leo tarehe 16 Mei, 2021 na kushirikisha kata za Buziku (Halmashauri
ya Wilaya ya Chato), Bugarama (Halmashauri ya Wilaya ya Geita), Igunga (Halmashauri
ya Wilaya ya Igunga), Ligoma (Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru) na Kata ya Miuta
iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.
Amevitaka vyama vya siasa,
wagombea na wadau wa uchaguzi kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria
vya uvunjifu wa amani kwani jukumu la kulinda amani ni la kila mwananchi, hivyo
wahakikishe wanalinda amani iliyopo sasa kwenye majimbo na kata zinazofanya
uchaguzi huo.
Jaji Mst. Kaijage amesema Sheria
na Kanuni za Uchaguzi zimeweka mamlaka na taratibu zinazotakiwa kufuatwa iwapo
kutakuwepo na malalamiko yoyote wakati wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama vya
siasa na wagombea kufuata taratibu hizo ili kuuufanya uchaguzi huo ufanyike kwa
uhuru na haki.
Mweyekiti huyo wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi amewataka wapiga kura wote waliojiandikisha katika majimbo ya
Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na kata tano za Tanzania Bara kujitokeza
kupiga kura ili waweze kuwachagua wabunge na madiwani wanaowataka.
Amevitaka vyama vya siasa
wagombea na wafuasi wao kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi zimekamilika jana jioni
saa 12:00 hivyo hawaruhusiwi kufanya mikutano ya kampeni kuanzia muda huo na
hawaruhusiwi kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni kama vile
vipeperushi, bendera na mavazi.
“Pili upigaji kura utafanyika
katika vituo vya kupigia kura vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu
wa mwaka jana.Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa
saa 10:00 jioni.Iwapo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao walifika kabla
ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura, mtu yeyote
hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00
jioni”alisema Jaji Mst. Kaijage na kuongeza:
“Watakaoruhusiwa kupiga kura ni
wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye majimbo na
kata husika na wana kadi zao za mpiga kura.Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia
masharti ya Kifungu cha 61 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na
Kifungu cha 62 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imeruhusu
wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho
mbadala.”
“Mojawapo ya vitambulisho
mbadala ambavyo mpiga kura anaweza kutumia ni Passi ya Kusafiria, Leseni ya
Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (NIDA).Mpiga kura aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika ataruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala
iwapo tu atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina
lake lipo kwenye orodha ya wapiga kura anapokwenda kupga kura. Aidha majina
yake yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yafanane na yale yaliyopo
katika kitambulisho mbadala”
Jaji Mst. Kaijage amekumbusha
kuwa katika vituo vya kupigia kura kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye
ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokuwa na watoto
vituoni na kutakuwa na majalada ya nuktanundu katika vituo vya kupigia kura kwa
ajili ya watu wenye ulemavu wa kuona ili weweze kupiga kura wenyewe.
Alifafanua kuwa kwa wapiga kura
wenye ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada hayo wanaruhusiwa kwenda
vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.
Amewakumbusha wapiga kura
kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya mwaka jana yaliyokubaliwa na wahusika wote
vikiwemo vyama vya siasa, kuwa wapiga kura watatakiwa kuondoka vituoni mara tu
baada ya kupiga kura, hivyo Tume imewashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko
katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.
Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na Uchaguzi wa Udiwani katika kata tano za Tanzania Bara, itahusisha idadi ya wapiga kura watakaopiga kura 303,965 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na vituo vya kupigia kura vitakavyotumika kupigia kura ni vituo 793.