Tume yapitia rufaa tatu na kuamua kuwarejesha wagombea udiwani katika Uchaguzi Mdogo wa Desemba 17, 2022
Imewekwa: December 07, 2022
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepitia, kuchambua na kufanya uamuzi wa rufaa tatu na kuwarejesha wagombea Udiwani katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge na Udiwani unaotarajia kufanyika tarehe 17 Desemba mwaka 2022.
Uamuzi huo umefanywa na
kikao cha Tume kilichokaa tarehe 6 Desemba, 2022 baa da ya kupitia rufaa za wagombea
Udiwani zilizowasilishwa kufuatia baadhi ya wagombea Udiwani kutoridhika na maamuzi
ya Wasimamizi wa Uchaguzi.
Kwa
mujibu wa taarifa ya kikao hicho iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles, wagombea hao waliwasilisha
rufaa Tume kufuatia pingamizi walizowasilisha
baada ya uteuzi wa tarehe 30 Novemba, 2022 katika Kata 12 za Tanzania Bara.
Dkt. Charles alisema Tume
imekubali rufaa ya Ndugu Joseph Yunja Machiya kupitia ACT-WAZALENDO na
kumrejesha katika orodha ya wagombea wa Udiwani katika Kata ya Mwamalili,
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
“Tume imekubali rufaa ya Ndugu
Vitali Mathias Maembe kupitia ACT-WAZALENDO na kumrejesha katika orodha ya
wagombea wa Udiwani katika Kata ya Dunda, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.” alisema
Dkt. Charles na kuongeza kuwa:
“Tume imekubali rufaa ya Ndugu
Samwel Azaria Mnyellah kupitia NCCR-MAGEUZI na kumrejesha katika orodha ya
wagombea wa Udiwani katika Kata ya Majohe, Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam.”
Alifafanua kuwa Tume
imefikia maamuzi hayo kwa kuzingatia Kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi
ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 kikisomwa pamoja na kanuni ya 29(1), (2) na
30 (4) za Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani), 2020.
Alibainisha kuwa vifungu
hivyo vinatoa fursa kwa wagombea Udiwani kukata rufaa wanapokuwa hawajaridhika
na uamuzi wa Wasimamizi wa Uchaguzi kutokana na pingamizi zilizowasilishwa na
vinaipa Tume mamlaka ya kukubali au kutengua uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi.
Baada ya kuwarejesha
wagombea hao, Dkt. Charles alieleza kuwa Tume imewapongeza wagombea na vyama vyao
vya siasa ambao walifuata taratibu za kisheria katika kudai haki zao,
kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya kushiriki katika uchaguzi huu mdogo ili
kupata ridhaa ya wananchi na kuwa viongozi katika kata husika.
“Aidha Tume
inaendelea kuwakumbusha wadau wote wa uchaguzi kuzingatia na kufuata njia
sahihi zilizowekwa kisheria, ili kutatua changamoto zozote zinazojitokeza
katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi huu mdogo, ikiwemo kufuata
maadili ya uchaguzi ambayo vyama vyote vya siasa viliridhia kuyafuata wakati wa
uchaguzi.” alisema Dkt. Charles na kuongeza kuwa:
“Kwa upande
mwingine Tume pia inawakumbusha wasimamizi na watendaji wote wa uchaguzi katika
maeneo husika kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, maelekezo ya Tume katika
kuendesha na kusimamia uchaguzi huu.”
Alisema kutokana na uamuzi huo, Uchaguzi huu Mdogo wa Udiwani
unafanyika katika kata Saba
ambazo ni Majohe (Dar es Salaam CC) Dar es Salaam, Mndumbwe (Tandahimba DC)
Mtwara, Njombe Mjini (Njombe TC) Njombe, Dunda (Bagamoyo DC) Pwani, Mwamalili
(Shinyanga MC) Shinyanga, Mnyanjani (Tanga CC) Tanga, na Vibaoni (Handeni DC)
Tanga.
Kata hizo saba zitaungana
na Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Amani,
Wilaya ya Mjini, Zanzibar utakaofanyika siku ya Jumamosi, tarehe 17
Disemba, 2022 ambapo Upigaji Kura utafanyika katika vituo vilivyotumika
wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
Ili kufanikisha uchaguzi huo, Dkt. Mahera alisema Tume inatoa rai kwa wananchi wote wa maeneo hayo kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.