Elimu ya Mpiga Kura
Elimu ya Mpiga Kura ni elimu ambayo hutolewa kwa wananchi wote kwa lengo la kuwawezesha kuelewa kuhusu Sheria, Kanuni, Taratibu za mchakato mzima wa Uchaguzi, wajibu wao na umuhimu wa kushiriki katika Uchaguzi, ni elimu isiyokuwa na hisia, ubaguzi wala itikadi za kisiasa.
Elimu ya Mpiga Kura inalenga kuwahamasisha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba katika kujitokeza na kushiriki kuchagua viongozi wao watakao waongoza ili kujenga Demokrasia na Utawala Bora nchini.
Dhana hii ya Elimu ya Mpiga Kura inahusisha pia usambazaji wa taarifa, vielelezo na vipindi mbalimbali katika Vyombo vya Habari ambavyo vinalenga kuwaelimisha Wananchi juu ya mchakato wa Uchaguzi. Mchakato huu unahusisha Uandikishaji wa Wapiga Kura, Ugawaji wa Majimbo, Uwekaji wazi Daftari, Kampeni, utaratibu wa Kupiga Kura na vituo vya Kupiga Kura.
Elimu ya Mpiga Kura hutolewa kuhakikisha kuwa Wapiga Kura wanahamasika na wanakuwa tayari kwa hiyari yao, kwa ufahamu wao na kwa kujiamini kwao kushiriki katika mchakato wa Uchaguzi wakiwa na mtizamo wa kukuza demokrasia.
Umuhimu wa Elimu ya Mpiga Kura
Elimu ya Mpiga Kura ni nyenzo na kielelezo muhimu katika kumuwezesha kila mwananchi kuelewa kuhusu mchakato wa Uchaguzi na nafasi yake katika kupiga kura. Elimu hii huwajengea ufahamu/uelewa wananchi kuhusu haki na wajibu wao kushiriki katika mchakato wa Uchaguzi wakiwa na taarifa kamili na sahihi juu ya michakato yote ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani
Mamlaka ya Tume kutoa Elimu ya Mpiga Kura
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kifungu cha 4C kimeipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi mamlaka ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima, Kuratibu na kusimamia Taasisi, Asasi na watu wanaotaka kutoa Elimu ya Mpiga Kura.
Kutokana na matakwa ya Sheria iliyotajwa hapo juu, Tume hutoa Elimu ya Mpiga Kura pia kwa kushirikiana ha Asasi za Kiraia katika kutoa Elimu hiyo.
Ushirikiano na Asasi za Kiraia katika utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura
Aidha, Tume imekuwa ikishirikiana na Asasi za kiraia katika kuelimisha umma kuhusu mchakato wa Uchaguzi kwa kutoa Vibali kwa Asasi za kiraia kushiriki kutoa Elimu ya Mpiga Kura. Aidha, Tume ina utaratibu wa kuzialika Asasi hizo zinazokusudia kutoa elimu hiyo ambapo huwasilisha maombi na zana zao za Elimu ya Mpiga Kura ili:
i. Kupitia na kuidhinisha zana na nyenzo zote za Elimu ya Mpiga Kura zitakazotumiwa na Asasi za kiraia na wadau wote wanaojihusisha na utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura;
ii. Kupitia na kuidhinisha mipango (program) yote iliyoainishwa na Wadau wa utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura;
iii. Kufuatilia na Kuratibu mpango (program) wa utaoaji wa Elimu ya Mpiga Kura ili kuhakikisha kwamba zinatolewa kwa umakini, usahihi bila kupotosha Wananchi na zinawafikia walengwa wote waliokusudiwa; na
iv. Kufanya tathmini ya zoezi zima la utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kuona iwapo Elimu hiyo imetolewa ipasavyo na imewafikia walengwa.
Vigezo vinavyotumika katika kutoa vibali ni pamoja na Asasi:-
- Kuwa na usajili kwa mujibu wa Sheria za Tanzania;
- Kuwa imefanya kazi Tanzania si chini ya miezi 6 toka kusajiliwa;
- Miongoni mwa Watendaji wake wakuu, Wawili wanapaswa wawe Watanzania;
- Kuwa haina taarifa za kuvuruga amani au kuchochea fujo; na
- Kuwa tayari kujigharamia katika kutoa Elimu ya Mpiga Kura.
Aidha, Asasi inapowasilisha maombi hayo inatakiwa kuambatanisha:-
- Cheti cha Usajili;
- Katiba ya Asasi;
- Majina ya Viongozi wa juu wa Asasi;
- Anuani kamili ya makazi (Physical Address) na Namba za simu za Ofisini na Viongozi;
- Zana za Elimu ya Mpiga Kura (Vijarida, Vipeperushi, Mabango, Vipindi vilivyorekodiwa, T-shirt n.k.); na
- Ratiba itakayoonyesha tarehe na mahali watakapotoa Elimu ya Mpiga Kura katika halmashauri husika.
Tume imekuwa ikishirikiana na Wadau mbalimbali wa Uchaguzi katika kuhakikisha kila mwananchi anapata Elimu ya Mpiga Kura. Wadau hao ni pamoja na;
- Wapiga Kura
- Vyama vya Siasa
- Asasi za Kidini (FBOs)
- Asasi za Kiraia (CSOs)
- Vyombo vya Habari
- Wanawake
- Vijana
- Jumuiya za Watu wenye Ulemavu
- Taasisi za Serikali
- Asasi za Kijamii (CBOs)
- Wadau wa Maendeleo
- Taasisi za Elimu
Ili Elimu ya Mpiga Kura iweze kutolewa na kuleta mafanikio ni muhimu kufanya uchambuzi na kutambua makundi ambayo yanalengwa kupatiwa elimu hiyo. Aidha, nyenzo na Vifaa vitakavyotumika kufikisha ujumbe uliokusudiwa ni muhimu pia kutambuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeyagawa makundi haya maalum katika sehemu kuu nne kama ifuatavyo:
- Makundi yaliyojitenga kutokana na sababu za kijiografia;
- Makundi yatokanayo na sababu za kimaumbile;
- Makundi ya wasiojua kusoma na kuandika;
- Wanawake na Vijana
Makundi yanayotokana na sababu za kijiografia na shughuli za kiuchumi
Makundi yanayotokana na sababu za kijiografia ni pamoja na wafugaji, wawindaji na wakulima. Vilevile, makundi haya ni ya watu ambao wanategemea kilimo, ufugaji na uwindaji.
Katika utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kwa kundi hili ni muhimu kuzingatia misimu yao ya kilimo na ufugaji kwa kuwa ni watu wanaohama kutoka eneo moja kwenda lingine kutegemeana na hali ya hewa.
Makundi yatokanayo na sababu za kimaumbile
Makundi haya ni yale yanayojumisha watu wenye ulemavu wa namna mbali mbali kama vile wasioona, wenye ulemavu wa kusikia, walemavu wa ngozi na wenye ulemavu wa viungo.
Makundi haya yanahitaji umakini zaidi katika kuwahudumia kwa kuzingatia maumbile yao, mfano kutumia lughaza alama na nukta nundu.
Makundi ya wasiojua kusoma na kuandika
Kundi hili ni la wapiga kura wasiojua kusoma na kuandika, ili kufikisha ujumbe katika kundi hili ni muhimu kutumia picha na maelezo ili kuweza kuwapa ufahamu kuhusu haki na wajibu wao kushiriki katika mchakato mzima wa Uchaguzi ili kuwa na taarifa kamili na sahihi za michakato yote ya Uchaguzi.
Wanawake na vijana wameanishwa kuwa ni makundi maalumu kutokana na na baadhi ya Wanawake kunyimwa haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi kwa kuzuiliwa na waume zao kutokana na mfumo dume. Aidha, Vijana wengi wamekuwa wakizuiliwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uchaguzi na kutumiwa na wanasiasa kuvuruga amani kwa masilahi ya wanasiasa, yote hayo yamefanyika kutokana na uelewa finyu wa haki zao za msingi za kushiriki katika Uchaguzi.
Njia za utoaji Elimu ya Mpiga Kura
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikitekeleza mkakati wa kutoa Elimu ya Mpiga Kura endelevu kwa kutumia njia zifuatazo:
- Mikusanyiko rasmi ya watu: Tume inatumia maonyesho ya Sabasaba, Nanenane, Mikutano ya Serikali za Mitaa (ALAT) na wiki ya Vijana kwa kutoa Elimu ya Mpiga Kura ana kwa ana au kuwapatia vijitabu na vipeperushi vyenye kuonyesha aina mbali mbali za michakato ya Uchaguzi.
- Mikutano na wadau: Tume inatumia mikutano na wadau mbalimbali katika kutoa elimu, Aidha imekuwa ikiandaa mikutano katika shule mbalimbali za sekondari kwa lengo la kuwaelimisha wapiga kura watarajiwa kuhusu shughuli za Tume na michakato ya Uchaguzi ili kuwahamasisha kushiriki katika michakato ya Uchaguzi.
- Vipindi vya redio na Runinga: Tume inaandaa na kutekeleza programu ya kushiriki katika vipindi mbali mbali vya redio na television ili kuweza kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria na kanuni mbali mbali za Uchaguzi.
- Makala za magazeti: Tume inaandaa makala mbalimbali katika magazeti mbalimbali lengo likiwa ni kutoa habari na kuelimisha umma kuhusu Sheria na taratibu za uendeshaji Uchaguzi.
- Mitandao ya kijamii; Tume pia imekuwa ikitumia mitandao ya kijamii katika kutoa habari za kuelimisha na kufahimisha.
- Vijitabu, vijarida na vipeperushi: Tume pia imekuwa ikiandaa vijitabu na vijarida mbali mbali ambavyo huvigawa kwa wananchi bure lengo likiwa ni kuwapatia uelewa kuhusu taratibu za Uchaguzi.
Katika kutoa Elimu ya Mpiga Kura Tume hutumia zana zifuatazo:
- Vijitabu;
- Vijarida;
- Vipeperushi;
- Mabango;
- Matangazo ya Runinga na Redio na Magazeti katika kuelimisha wananchi.