Wasimamizi wa Uchaguzi Mdogo watakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu
Imewekwa: October 03, 2018Wasimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Oktoba 13 mwaka huu katika jimbo la Liwale na kwenye Kata 37 za Tanzania Bara wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na Kanuni za uchaguzi.
Makamu Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk ameyasema
hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa
Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye
uchaguzi.
Jaji Mbarouk amewataka
Wasimamizi hao kufanya kazi kwa ufanisi, uhuru, uwazi na bila kuegemea
upande wowote ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu.
Amesema uchaguzi ni
mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na
kuzingatiwa akisisitiza kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi
mzuri wenye ufanisi usio na malalamiko au vurugu.
“ Tunakutana hapa ili kwa
pamoja tubadilishane uzoefu, tujadili namna ya kufanikisha zoezi la uchaguzi
lakini pia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza
katika hatua zote za uchaguzi, natumaini mtatumia fursa hii kubadilishana
uzoefu katika kutekeleza jukumu hili lililo mbele yenu” Amesema Jaji Mbarouk.
Jaji Mbarouk ametoa wito
Wasimamizi hao waepuke madhara yanayotokana na ukiukaji wa Sheria, Kanuni na
taratibu za Uchaguzi akisisitiza kwamba katika kipindi hiki chaguzi
zinafanyika katika mazingira ambayo yana hamasa kubwa ya Kisiasa, kutoaminiana
na wakati mwingine kutawaliwa na mihemko ambayo imekuwa chanzo cha uvunjifu wa
amani.
Aidha, amewaeleza
Wasimamizi hao kuwa wameaminiwa na kuteuliwa katika nafasi hizo kwa kuwa wanao
uwezo mkubwa wa kufanya kazi hivyo wajiamini na kujitambua.
Ametoa wito kwa
Wasimamizi hao kuhakikisha kwamba wanayaelewa vema maeneo yao ya kazi na wanawatumia
vyema wasaidizi walio nao katika maeneo yao ya kazi kwa matokeo bora.
“Naomba mjue mna jukumu
la kuimarisha imani ya wananchi pamoja na wadau wote wa uchaguzi kwa Tume.
Hivyo mfanye kazi kwa ufanisi wa hali ya juu, bila kuegemea upande wowote.Kufanya
kazi kwa uhuru na kwa uwazi kutasaidia kudumisha amani katika maeneo yenu ya
Uchaguzi” Amesema.
Kuhusu kufanyika kwa
Uchaguzi huo mdogo Oktoba 13 mwaka huu, Jaji Mbarouk amesema kuwa kwa
kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi,
Sura 343 kikisomwa pamoja na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Serikali za Mitaa,
Sura 292, ni jukumu la Tume kusimamia, kuendesha na kuratibu uchaguzi wa kujaza
nafasi zilizo wazi.
Amesema kwa nyakati tofauti Tume imepokea
taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa
kuzingatia Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343
aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Ubunge katika jimbo la Liwale.
Pia amefafanua kuwa
Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, ambaye kwa kuzingatia masharti ya
kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali ya Mitaa, Sura, 292 alitoa
taarifa ya uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 37 kutoka katika
Halmashauri 27 zilizopo katika Mikoa 13 ya Tanzania Bara.
Katika hatua nyingine
Makamu Mwenyekiti huyo wa NEC Jaji
Mbarouk Salim Mbarouk ameeleza kuwa jumla ya wagombea 6 waliteuliwa kugombea
ubunge katika jimbo la liwale ambapo mgombea mmoja alijitoa baada ya uteuzi huo
kukamilika.
Ameongeza kuwa katika Kata 37 za Tanzania Bara jumla ya wagombea 56 waliteuliwa kugombea udiwani katika Kata hizo.