MKURUGEZI WA UCHAGUZI ATOA TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UGAWAJI WA MAJIMBO YA UCHAGUZI WA WABUNGE
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UFAFANUZI KUHUSU UGAWAJI WA MAJIMBO YA UCHAGUZI WA WABUNGE
Kwa mujibu wa Ibara ya 75(1)(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo yenye mamlaka ya kuchunguza mipaka na kugawa majimbo ya Uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi wa Wabunge na siyo chombo kingine chochote.
Itakumbukwa kuwa tarehe 22/01/2010, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa taarifa katika Vyombo vya Habari ikielezea nia yake ya kuchunguza mipaka na kugawa Majimbo kwa ajili ya Uchaguzi wa Wabunge. Katika maelezo yake, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilibainisha Vigezo na Utaratibu utakaotumika katika kuleta maombi kwa ajili ya kurekebisha mipaka au kugawa Majimbo. Taarifa hiyo pia ilieleza hatua zitakazofuata baada Tume kupokea maombi.
Katika utaratibu ulioainishwa wa kuleta maombi ya kurekebishiwa mipaka au kugawanya majimbo, Tume ilizielekeza Halmashauri kufanya vikao rasmi na kushirikisha wadau wote katika eneo la Halmashauri husika ili kupata maoni na mapendekeza kutoka kwa wadau na kisha Mkurugenzi wa Halmashauri husika kuwasilisha maoni na mapendekezo ya wadau hao katika Kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa. Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kinatakiwa kuchambua maoni na mapendekezo hayo na kisha kuyawasilisha Tume. Taarifa ilieleza mwisho wa kupokea mapendekezo hayo ni tarehe 28/02/2010.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kupitia magazeti mbalimbali imeona baadhi ya Halmashauri zimechapisha mapendekezo ya ugawaji wa Majimbo mapya kwenye magazeti, kitu ambacho kinawapa picha Wananchi kuwa Majimbo hayo yameshagawiwa tayari.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kuwaarifu Wananchi wote kwamba majimbo hayo bado hayajagawiwa kwa kuwa Chombo pekee kinachohusika na ugawaji wa Majimbo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Aidha, Tume inapenda kuwaarifu wananchi wote kuwa bado inaendelea kupokea maombi ya mapendekezo ya kurekebisha mipaka au kugawa majimbo kutoka kwenye Halmashauri mbalimbali. Tume ikishapokea maombi hayo itayafanyia uchambuzi kulingana na vigezo na utaratibu uliowekwa. Majimbo yatakayokidhi vigezo yatashindanishwa tena kwa kuzingatia nafasi za viti zitakazoweza kuongezwa katika ukumbi wa Bunge.
Tume inawaomba Wananchi wafahamu kuwa mpaka sasa hakuna ugawaji wa Majimbo wowote ambao umeshafanyika. Tume itafanya ugawaji wa majimbo baada ya kupokea na kuyachambua maombi kutoka kwa Makatibu Tawala wa Mikoa. Tume ikikamilisha zoezi hilo itawatangazia wananchi na kuwaarifu kuhusu majimbo mapya yatakayoanzishwa.
Tume inawaomba Wananchi wote kuvuta subira ili mchakato wa zoezi hili uweze kutekelezwa kwa mujibu wa Sheria za Nchi na taratibu zilizowekwa.
(Rajabu R. Kiravu )
MKURUGENZI WA UCHAGUZI