HOTUBA YA MAKAMU MWENYEKITI KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI
HOTUBA YA MAKAMU MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI, MHE. JAJI OMAR O. MAKUNGU KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI ULIYOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA PARADISE CITY HOTEL JIJINI DAR-ES-SALAAM TAREHE 1/12/2009.
Waheshimiwa Wahariri wa Vyombo vya Habari,
Waheshimiwa Makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
Mkurugenzi wa Uchaguzi,
Watendaji wa Tume,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.
Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisheni wote katika mkutano huu muhimu wa kubadilishana mawazo na kupeana taarifa kuhusu Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Ninatambua kwamba mna wajibu na majukumu mengi na mazito yanayowakabili lakini kwa kutambua umuhimu wa mkutano huu mmeweza kufika tena kwa wakati
Tume inafarijika sana kukutana nanyi siku ya leo na inawashukuru sana kwa moyo mliyoonyesha wa kuhudhuria Mkutano wetu.
Mtakumbuka kwamba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikutana nanyi tarehe 12/12/2007 katika Ukumbi wa Mikutano wa PPF Tower ambapo tuliwaeleza kuhusu mchakato wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Kwanza. Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Kwanza lilifanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na ushirikiano wenu mzuri mlioonyesha wakati wa zoezi hilo pamoja na michango mizuri ya mawazo ambayo Tume iliipata kutoka kwa wadau mbali mbali vikiwemo Vyombo vya Habari.
Waheshimiwa Wahariri wa Vyombo vya Habari,
Leo Tume inakutana nanyi kwa mara nyingine tena ili kuwapa taarifa kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao. Hii ni kutokana na Tume kutambua na kuthamini michango mbalimbali ya Wadau wa Uchaguzi mkiwemo ninyi Wahariri wa Vyombo vya Habari pamoja na fursa mlizonazo katika kufikisha habari na taarifa mbali mbali kwa wananchi wote wa Tanzania. Ni dhahiri kwamba Vyombo vya Habari ni mhimili mkubwa katika mchakato wa Uchaguzi kwa kuwa vina uwezo na nyenzo muhimu za kuwawezesha wananchi kupata taarifa mbali mbali zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi.
Vyombo vya Habari vile vile vina uwezo wa kuwafikia wananchi wote popote pale walipo nchini hasa ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya maeneo katika nchi yetu ambayo yanakabiliwa na matatizo ya kukosa mawasiliano kutokana na uduni wa miundombinu pamoja na umbali. Wahariri wa Vyombo vya Habari kwa kutumia taaluma zenu mnao uwezo na utaalamu wa kuhamasisha na kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa wananchi wote kulingana na mahitaji yao, matarajio, matakwa na hali ya mahali walengwa walipo.
Vile vile wananchi wana imani kubwa na Vyombo vya Habari na wanavitegemea sana Vyombo vya Habari katika kupata habari na kuelimishwa kuhusu masuala yanayohusu maisha yao na Taifa kwa ujumla. Kama mnavyofahamu, tumebakiwa na kipindi cha miezi kumi na moja tu ili kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ujao.
huu sasa ni wakati muafaka wa Tume kukaa pamoja na Wadau na kujadili kuhusu namna ya kufanikisha Uchaguzi huo. Ni katika kutambua umuhimu huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaheshimu na kuenzi sana uwepo wenu hapa siku ya leo na umuhimu wa Vyombo vya Habari katika kufikisha habari na taarifa mbali mbali kwa wananchi zinazohusu wajibu wao wa kushiriki katika Uchaguzi na kuwaelimisha kuhusu kutumia haki yao ya kikatiba na ya msingi ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.
Katika Mkutano wetu wa leo, Tume inatarajia kupata mawazo na ushauri wenu wa jinsi tutakavyoweza kuboresha na kufanikisha zaidi Uchaguzi Mkuu ujao hasa ikizingatiwa kwamba baada ya kumalizika zoezi la Awamu ya Pili ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hakutakuwa na uandikishaji mwingine hadi utakapomalizika Uchaguzi Mkuu ujao.
Vile vile, ziko changamoto mbalimbali zinazoikabili Tume ikiwemo baadhi ya watu kupoteza kadi zao za kupiga kura. Ili uchaguzi ulio wazi, huru na wa kidemokrasia uweze kufanyika, kila mwananchi mwenye sifa kisheria anatakiwa kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuitunza kadi yake hadi siku ya Uchaguzi itakapowadia.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Kwanza ulikwisha kamilika na sasa Tume iko katika mchakato wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili.
Waheshimiwa Wahariri wa Vyombo vya Habari,
Kama ilivyofanyika katika Uchaguzi wa 2005, Tume inawaandikisha Wapiga Kura wote wenye sifa Kisheria na ambao wana miaka 18 na kuendelea na wale ambao watakuwa wamefika miaka 18 ifikapo mwezi Oktoba 2010. Lengo ni kuwawezesha wananchi wote kutumia haki yao ya kikatiba kupiga Kura na kuwachagua viongozi wao wanaowataka.
Tume vile vile inawaandikisha wale wote wenye sifa ambao hawakupata fursa ya kujiandikisha wakati wa Uanzishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Kwanza. Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili vile vile linakwenda sambamba na utoaji wa Kadi mpya kwa wale wote waliopoteza au kuharibikiwa na kadi zao za kupiga kura.
Watu ambao watapenda kusahihisha au kubadilisha taarifa zao zilizomo katika Daftari mfano wale ambao majina yao yalikosewa, au waliobadilisha majina kutokana na sababu mbali mbali mfano walikuwa hawajaolewa wakati walipojiandikisha na sasa wameolewa na wangependa kubadili majina yao, wanapewa fursa ya kufanya hivyo.
Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili linahusisha pia kuhamisha taarifa za Wapiga Kura waliohama kutoka Jimbo/Kata moja kwenda Jimbo/Kata nyingine na kuwaondoa kwenye Daftari Wapiga Kura wote waliofariki na waliopoteza sifa kisheria.
Waheshimiwa Wahariri wa Vyombo vya Habari,
Kufanikiwa kwa zoezi hili la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili na Uchaguzi Mkuu ujao, kunategemea wananchi wote kupewa taarifa sahihi zisizopotoshwa na zisizokuwa na itikadi za kisiasa. Taarifa zenye kuzingatia viwango tofauti vya uelewa wa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya watu hawajui kusoma na kuandika. Vile vile wananchi wanatakiwa kupewa taarifa kwa wakati ili kutoa fursa kwa wao kujiandaa na hatimaye kushiriki katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Sambamba na zoezi la awamu ya pili ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, Tume imeendelea kuboresha mifumo mbali mbali ya Kiteknolojia ili kuboresha na kufanikisha Uchaguzi huo.
Katika kuboresha mifumo hiyo ya Kiteknolojia, wananchi wataweza kupata taarifa zao zilizoko kwenye “Database” kwa kutumia simu za kiganjani kupitia ujumbe mfupi wa maneno (sms) Tume na kupatiwa taarifa wanazotaka bila wao kulazimika kufika Tume wenyewe.
Waheshimiwa Wahariri wa Vyombo vya Habari,
Tume imeandaa Mkakati wa utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura ambao umeainisha njia na mbinu mbalimbali zitakazotumika kutoa taarifa kwa wananchi wote na kuwahamasisha kujitokeza kushiriki katika Uchaguzi. Tume pia imefanya utafiti wa kubaini vikundi mbalimbali vya sanaa pamoja na Asasi za Kiraia ambazo zinajihusisha na uhamasishaji wananchi na kutoa Elimu ya Mpiga Kura. Lengo ni kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapata taarifa zitakazomuwezesha kushiriki katika Uchaguzi.
Vile vile, Tume imefanyia kazi sheria za Uchaguzi na kupendekeza mabadiliko mbalimbali na kutoa mapendekezo ambayo yamewasilishwa Serikalini. Tume pia, inakusudia kuangalia mipaka ya Majimbo kwa kuzingatia matakwa ya sheria na vigezo vilivyowekwa kisheria.
Ili kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kushiriki katika mchakato wa uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inawaomba kufikisha taarifa zilizokusudiwa kwa wananchi wote kwa wakati na kuwahamasisha kujitokeza kushiriki katika mchakato wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Uchaguzi Mkuu ujao. Kama mnavyofahamu gharama za uchaguzi ni kubwa na Elimu ya Mpiga kura ikiwa ni sehemu muhimu katika mchakato wa uchaguzi vile vile ina gharama kubwa.
Hivyo Tume inawaomba kutoa mchango wenu wa kuhamasisha na kuelimisha wananchi waweze kujitokeza siku ya kupiga kura. Mtakapokuwa mnatekeleza majukumu mengine ya kitaifa Tume inawaomba kutumia fursa hiyo kutoa ujumbe wa Uchaguzi na umuhimu wa wananchi kushiriki katika Uchaguzi.
Tume vile vile inaviomba Vyombo vya Habari kuwahamasisha wananchi wote kutoa taarifa sahihi kuhusu watu ambao wameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lakini sasa wamefariki ili taarifa zao ziondolewe kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Wananchi wote pia wanaombwa kutunza Kadi zao za kupiga Kura vizuri kwani mtu hataruhusiwa kupiga kura kama atakuwa hana kadi ya kupiga kura.
Kwa kumalizia ninapenda tena kuwashukuru wote kwa kuhudhuria Mkutano huu na Tume inaahidi kuyachukua mawazo yote yatakayotolewa hapa na kuyafanyia kazi ili kufanikisha na kuleta ufanisi katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ninatangaza kuwa Mkutano wetu umefunguliwa.